Bility akata rufaa uamuzi wa kumzuia kuwania Fifa

Bility Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ni wagombea watano pekee walioidhinishwa kuwania

Mkuu wa shirikisho la soka la Liberia, Musa Bility, amekata rufaa kwenye mahakama ya kuatatua mizozo ya michezo (Cas) akilalamikia kuzuia kuwa mgombea uchaguzi wa urais Fifa.

Bw Bility alizuiwa kuwania na kamati ya uchaguzi ya Fifa kwa madai kwamba hakupita vigezo vya maadili.

“Uamuzi wa Fifa si wa haki, unaudhi na kusikitisha,” Bility alisema kupitia taarifa.

“Nimekata rufaa kwa Cas nikiwahimiza washughulikie rufaa yangu kwa dharura.”

Bw Bility, mwenye umri wa miaka 48, amekosoa uhalali wa vigezo vilivyotumiwa, na pia ameitaka Fifa kufanya wazi matokeo ya uchunguzi kuhusu kila mgombea kwa mashirikisho yote 209 ya soka, badala ya kuyafungia.

Uchaguzi wa kuamua mrithi wa raia anayeondoka Sepp Blatter utafanyika Februari 26.