Real Madrid waondolewa Copa del Rey

Denis Cheryshev Haki miliki ya picha Getty
Image caption Denis Cheryshev alifungia Real bao la kwanza

Klabu ya Real Madrid imefurushwa kutoka michuano ya Copa del Rey kwa kumchezesha mchezaji ambaye hakufaa kuchezeshwa wakati wa mechi yao dhidi ya Cadiz Jumatano.

Mchezaji huyo, Denis Cheryshev, ndiye aliyewafungulia Real ukurasa wa mabao wakati wa mechi hiyo ambayo walishinda 3-1.

Winga huyo wa Urusi alifaa kuwa akitumikia marufuku, aliyopewa alipokuwa Villarreal kwa mkopo.

Lakini yeye na klabu yake ya Real, wanasema hawakujuzwa hilo kabla ya mechi hiyo.

Klabu hiyo imesema itachukua “hatua ifaayo” kuhakikisha matokeo “ya kuridhisha”. Cheryshev, 24, aliondolewa uwanjani muda mfupi baada ya mapumziko, baada ya Real kugundua kosa hilo.

Real wameshinda kombe hilo mara 19, majuzi zaidi ikiwa 2014.

Jaji wa Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF) Rubio Sanchez alisema ushindi wa mechi hiyo sasa utakabidhiwa Cadiz.

Real pia wametakiwa kulipa faini ya euro 6,001 (£4,300).

Gazeti la Uhispania la Marca limeripoti kuwa Real watakata rufaa uamuzi huo.