CAF yairuhusu Sierra Leone kuandaa mechi

Sierra Leone Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sierra Leone ilizuiwa kuandaa mechi kutokana na mkurupuko wa ugonjwa wa Ebola

Shirikisho la soka barani Afrika (Caf) limesema Sierra Leone sasa iko huru kuwa mwenyeji wa mechi za kimataifa na kanda.

Hii inafuatia uamuzi wa Shirikisho la Afya Duniani (WHO) kutangaza taifa hilo kuwa huru kutoka kwa ugonjwa wa Ebola mwezi jana, Caf imesema kupitia taarifa.

Nchi hiyo ya Afrika Magharibi ilipigwa marufuku kuandaa mechi za kandanda Agosti 2014 kwa kufuata ushauri wa WHO baada ya kutokea kwa mkurupuko wa ugonjwa wa Ebola eneo hilo.

Watu zaidi ya 10,000 waliuawa na ugonjwa huo tangu Desemba 2013, wengi wao wakifariki Liberia, Guinea na Sierra Leone.

Katika mataifa hayo matatu, ni Guinea pekee sasa ambayo hairuhusiwi kuandaa mechi za Caf, kwani haijatangazwa kuwa huru kutoka kwa Ebola na WHO.