Schweinsteiger kufungiwa mechi 3

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Bastian Schweinsteiger

Kiungo wa Manchester United Bastian Schweinsteiger yupo hatarini kufungiwa Mechi 3 za ligi kuu ya England baada ya kufunguliwa Mashitaka na Chama cha Soka cha England FA , kwa kosa la Kinidhamu.

Schweinsteiger, mwenye Miaka 31, anadaiwa kumpiga Beki wa West Ham Winston Reid kwa Mkono wa Kushoto walipokuwa wakigombea Mpira wa Frikiki katika Dakika ya 40 kwenye Mechi ya Ligi Kuu England iliyomalizika 0-0 Jumamosi iliyopita.

Schweinsteiger amepewa hadi Alhamisi Saa 9 Mchana kukana au kukubali Mashitaka.

Refa wa Mechi hiyo, Mark Clattenburg, hakulitaja tukio hilo lakini aliongea na Wachezaji wote Wawili baada ya tukio lenyewe.

Katika Taarifa yao, FA imesema kuwa tukio hilo lilipitiwa na Marefa Watatu tofauti ambao kila mmoja aliafiki lilistahili Kadi Nyekundu na ndio maana wakafungua Mashitaka dhidi ya Schweinsteiger.

Laiti kama Refa Mark Clattenburg angelilitaja tukio hilo kwenye ripoti yake ya Mechi basi FA isingekuwa tena na mamlaka ya kulipitia na kumshitaki.

Ikiwa Schweinsteiger atafungiwa Mechi 3 atazikosa Mechi za Ligi dhidi ya Bournemouth, Norwich City na Stoke City na kurejea kwenye Mechi na Chelsea.