Uganda Cranes wahusika kwenye ajali

Cecafa Haki miliki ya picha FUFA
Image caption Uganda walishinda 1-0 kwenye fainali ya Cecafa

Basi lililokuwa limebeba wachezaji wa timu ya taifa ya kandanda ya Uganda limehusika kwenye ajali ya barabarani wakirejea Kampala baada ya kukutana na Rais Yoweri Museveni.

Wachezaji wote wa Uganda Cranes na maafisa wa timu wote wako salama, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) ingawa wanne waliumia na kupokea huduma ya dharura.

Basi lililobeba timu hiyo liligonga teksi mwendo was aa tisa unusu alasiri katika barabara ya Kamokoli-Jami, karibu na mji wa Mbale baada ya tairi ya gurudumu la mbele la basi hilo kupata panchari.

Wachezaji hao, walikuwa wameenda kukutana na Bw Museveni mjini Soroti kaskazini mwa Kampala baada ya kushinda Kombe la Cecafa kwa kucharaza Rwanda kwenye fainali Jumamosi iliyopita.

Walioumia ni wachezaji Kezironi Kizito, Denis Okot Oola na Hassan Wasswa Dazo na afisa wa mawasiliano wa FUFA Ahmed Hussein.

“Juhudi zimefanywa kupata njia mbadala ya kusafirisha timu hadi Kampala,” taarifa ya shirikisho hilo imesema.