Roger Federer kucheza na Martina Hingis Rio

Federer Haki miliki ya picha Getty
Image caption Federer amesema ana furaha kucheza pamoja na Hingis

Nyota wa tenisi Roger Federer atashirikiana na bingwa wa zamani wa Wimbledon Martina Hingis kutoka Uswizi katika mashindano ya jinsia mchanganyiko Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016.

Federer, 34, na Hingis walicheza mara ya mwisho pamoja katika Kombe la Hopman nchini Australia 2001.

Bingwa huyo mara 17 wa Grand Slam amesema ana “furaha sana”.

"Nilimuenzi sana nilipokuwa mchanga. Niliamini alikuwa na kipaji adimu,” aliongeza Federer, ambaye ni mdogo wa Hingis kwa mwaka mmoja.

“Tuko karibu sawa kwa umri na alikuwa akishinda mataji ya Grand Slam nilipokuwa bado kituo cha taifa cha tenisi. Nilishangazwa sana na ustadi wake.”

Haki miliki ya picha AP
Image caption Hingis alitwaa taji la Wimbledon mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 16

Hingis, 35, alishinda mataji matano ya Grand Slam katika uchezaji wake, moja akilitwaa Wimbledon mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 16.

Alikuwa amestaafu mara mbili awali lakini akarejea mchezoni tena 2013 na amekuwa akifanikiwa mashindanoni.