Yaya Toure angekuwa mchezaji karate

Yaya
Image caption Toure alikuwa ameanza kucheza karate akiwa mtoto

Iwapo mambo yangefanyika tofauti, Yaya Toure wa Ivory Coast, ambaye alishinda tuzo ya BBC ya kila mwaka ya mchezaji bora Afrika kwa mara ya pili siku ya Ijumaa angekuwa mchezaji karate.

Huo ndio mchezo ambao kiungo huyo wa kati wa Manchester City alikuwa ameanza kucheza alipokuwa mtoto na huenda angefanya vyema na kusalia huko iwapo babake asingemzuia.

Alikwenda kujifunza karate kabla ya kuanza kucheza soka, Mory Toure, babake Yaya ameiambia BBC Sport.

Katika kipindi cha wiki moja, alifanya vyema na aliweza kuteuliwa kushiriki katika mashindano nchini Kenya.

Lakini, tamaa yake ilikatizwa na babake ambaye alimpiga marufuku Yaya kusafiri kwa kuwa alihofia angepata jeraha mbaya baada ya kujiunga na mchezo huo.

''Nilikuwa nikipigana sana na ndugu zangu, kwa hivyo babangu alisema ataniingiza katika mchezo ambao utanituliza, na mchezo wa karate ulifanya hivyo'',Yaya ameiambia BBCSport akitabasamu.

''Wakati mmoja nilimpeleka kijijini na kumuweka katika shule ya kujifunza Koran, kwa sababu ilikuwa wakati wa likizo',” alisema mzee huyo wa miaka 69 ambaye amestaafu baada ya kuhudumu kwa kipindi kirefu katika jeshi.

Wiki moja baadaye, alikuwa akiandika na kuzungumza Kiarabu. Mwalimu wake aliniita na kusema kuwa ni mwerevu sana. ''Tayari anaandika na hasahau unachomwambia''.

''Kwa sasa Yaya anazungumza Kihispania, Kirusi, na Kiingereza. Hawezi kuzungumza lugha yake ya Tawana, ijapokuwa hayo ni makosa ya wazazi wake,” Mory anacheka.

Toure ameweza kuzungumza lugha nyingi kutokana na safari zake za soka barani Ulaya, ambazo zilianza Ubelgiji mwaka 2001 na ambazo zimeshirikisha Ukraine, Ugiriki,Ufaransa, Uhispania na Uingereza.

Katika ziara hizo ameshinda mataji yasiyohesabika na klabu ya Olympiakos, Barcelona, Manchester City.

Mataji hayo ni pamoja na kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na Klabu Bingwa Duniani akiwa na Barcelona 2009.

Taji lake la kwanza lilijiri aliposhinda ligi ya Ivory Coast na ASEC Mimosa mwaka 2001.

Klabu hiyo ni maarufu kwa kuwalea na kuwachipuza wachezaji nyota nchini Ivory Coast akiwemo Gervinho, Salomon Kalou, Didier Zokora, Emmanuel Eboue na nduguye mkubwa wa Yaya, Kolo Toure.

Image caption Toure ameshinda tuzo ya BBC ya mchezaji bora Afrika mara ya pili

Lakini ni mchezaji mmoja aliyeteka zaidi macho ya Jean Marc Guillou, aliyekuwa mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa na ambaye aliongoza klabu hiyo miaka ya tisini.

''Kutoka wakati alipoanza kuichezea ASEC, wakati alipougusa mpira, Guillou alisema alikuwa mchezaji mzuri sana na kwamba aliamini Yaya angeshinda tuzo ya mchezaji bora Afrika wakati mmoja,” alisema Mory.

''Ameshinda taji hilo (tuzo ya mchezaji bora Afrika ya CAF) mara nne sasa''.

Anashikilia rekodi hiyo na Samuel Eto'o, lakini Toure anaweza kushinda rekodi hiyo wakati shirikisho la soka barani Afrika CAF litakapomtangaza mchezaji bora wa mwaka huu mwezi ujao.

Mchezaji huyo wa umri wa miaka 32 akiwa miongoni mwa wale wanaopigiwa upatu kushinda.

''Wakati Yaya anapofanya kitu anakifanya vyema zaidi, hataki kufeli,” amesema.

Licha ya kuwa na historia ya kijeshi, Mory anamsifu mamake Yaya, badala yake wenyewe kwa kumfaa sana Yaya.

Mory ana watoto 10, tisa wakiwa walizaliwa na mama yake Yaya na nduguye Kolo, ambaye alifariki mwaka 2001 wakati nyota huyo wa Manchester City alipokuwa kijana.

''Yaya ni jasiri kama mamaake'', alisema Mory. Na anaposema atafanya kitu, atafanya. Ni mwanamume jasiri''.

''Kolo alichukua tabia yangu, ni mkarimu na anapozungumza kuhusu watu ni myenyekevu kwa maneno yake''.

''Hapendi mgogoro na pia hapendi kutokuwepo kwa haki anapenda ukweli na mambo kuwa wazi. Pia anapenda mashindano, na nitakwambia hadithi, wakati alipokuwa shule mpinzani wake mkuu darasani alikuwa msichana''.

''Wakati msichana huyo alipoongoza darasa, yeye alikuwa wa pili. Lakini kila mara msichana huyo alipokuwa kwanza alimwambia umenishinda wakati huu, lakini wakati ujao nitakuwa wa kwanza''.

''Na wakati utakaofuata, unakuta atamshinda msichana huyo hata kama ni na nusu alama''.

Yaya hakushinda taji lolote na Manchester City mwaka 2015 lakini hata hivyo, mchezo wake mzuri ulitosha kwa FIFA kumuorodhesha kama mchezaji pekee wa Afrika katika kuwania taji la Ballon d'Or.

Uwezekano wake kushinda ni mdogo sana, lakini ana taji la pili la BBC kuongezea kwa lile aliloshinda mwaka 2013 na kumfanya kuwa mtu wa tatu kushinda taji hilo mara mbili baada ya aliyekuwa mchezaji wa Nigeria Nwankwo Kanu na Jay Jay Okocha.