Timu 16 kuchuana CHAN 2016 - Rwanda .

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Uwanja wa taifa wa Amahoro ndiyo mkubwa zaidi Rwanda ukiwa na uwezo wa kubeba mashabiki 25,000

Rais wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na Mkuu wa Kamati ya Ndani ya Maandalizi (LOC) ya Michuano ya Ubingwa wa Mataifa wa Afrika (CHAN), Vincent Nzamwita amesema kwamba viwanja vyote vinne vitakavyotumika kwa mashindano hayo, vipo katika hali nzuri tayari kwa mechi.

Michuano hiyo inayohusisha wachezaji wanaocheza Ligi za nchini mwao pekee, inatarajiwa kuanza Januari 16 hadi Februari 7.

Nzamwita amesema kazi za ukarabati katika viwanja vya Amahoro na Nyamirambo mjini Kigali tayari imekamilika.

Viwanja hivyo ni pamoja na Huye na Umuganda (Rubavu) vitatumika kwa michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika ambayo itashirikisha timu 16 za Afrika.

Mara ya mwisho Rwanda kuandaa mashindano makubwa ya Afrika ilikuwa ni mwaka 2011 ilipokuwa mwenyeji wa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Afrika, ambayo mwishoni timu nne ikiwemo Amavubi, ziliiwakilisha Afrika katika fainali za dunia nchini Mexico mwaka huo.

Image caption Rwanda imepangwa Kundi A pamoja na Ivory Coast, Morocco na Gabon

Uwanja wa taifa wa Amahoro ndiyo mkubwa zaidi Rwanda ukiwa na uwezo wa kubeba mashabiki 25,000, ukifuatiwa na Huye (mashabiki 10,000), Nyamirambo (mashabiki 7,000) na Umuganda (mashabiki 5,200).

Rwanda imepangwa Kundi A pamoja na Ivory Coast, Morocco na Gabon, wakati Kundi B lina timu za DRC, Ethiopia, Cameroon na Angola, Kundi C kuna Tunisia, Guinea, Niger na Nigeria na Kundi D kuna Zimbabwe, Zambia, Uganda na Mali