Wayne Rooney awaasa wachezaji wenzake

Van Gaal Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Van Gaal amekabiliwa na shinikizo kutokana na klabu hiyo kutoandikisha matokeo mazuri

Nahodha wa Manchester United Wayne Rooney amewashauri wachezaji wenzake kukaza buti ili kuokoa kibarua cha meneja wao Louis van Gaal.

Kufuatia kutoshinda katika Mechi 6 zilizopita na kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kibarua cha Van Gaal kimekuwa kwenye hatari kubwa.

Klabu hiyo imeporomoka hadi nafasi ya 5 kwenye Ligi Kuu England na kujikuta wakiwa na Pointi 9 nyuma ya vinara Leicester City,

Rooney amenukuliwa akisema: "Hatujashinda katika wiki chache zilizopita na ni kawaida kupoteza kujiamini. Inabidi turejeshe imani kwani tuna michezo migumu na tunahitaji tuwe bora zaidi. Si kitu chema kufungwa kila mchezo. Ni ngumu kwa wachezaji. Tunaumia kwani sisi ni watu wa fahari na tunajionea fahari kuichezea Manchester United."