Man City ndio wenye nguvu zaidi - Pellegrini

City Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Manchester City kwa sasa wamo nambari tatu ligini

Meneja wa Manchester City Manuel Pellegrini anaamini timu yake ndiyo yenye nguvu zaidi katika Ligi ya Premia, wachezaji wake wote wakiwa sawa.

City kwa sasa wamo nambari tatu ligini, alama sita nyuma ya viongozi Leicester baada ya kushindwa 2-1 na Arsenal Jumatatu.

Nahodha wao Vincent Kompany, 29, atarejea kikosini baada ya kukosa mechi tisa. Mshambuliaji wao Sergio Aguero naye amekosa michezo 11 kutokana na jeraha.

“Tumo kwenye mashindano yote na tumefanya hivyo licha ya kukosa wachezaji wetu muhimu,” amesema Pellegrini.

"Lakini, bila shaka, wachezaji wetu wote wakiwa sawa na wakicheza kila mechi, timu yetu ndiyo yenye nguvu zaidi.”

Difenda wao Pablo Zabaleta na kiungo wa kati Fernando pia wanarejea baada ya kuuguza majeraha.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Kompany anarejea baada ya kukosa mechi tisa ligini

Hata hivyo, wameonekana kumkosa zaidi Kompany.

City walifanikiwa kumaliza mechi saba bila kufungwa Ligi Kuu ya Uingereza wakiwa na Kompany lakini baada yake kuumia, wamefanikiwa kumaliza mechi moja pekee kati ya sita bila kufungwa goli.

“Inaonekana kana kwamba tuko kwenye mzozo lakini hatuko kwenye mzozo. Kompany ndiye nahodha, na huwezi kuwa nahodha wa timu kubwa iwapo wewe si mchezjai muhimu,” amesema Pellegrini.

"Tunamhitaji Vincent, lakini timu hii haimtegemei mchezaji mmoja pekee.”

City watakutana na Sunderland Jumamosi.