Aston Villa kutafuta mshambuliaji wa Chelsea

Remy Haki miliki ya picha Getty
Image caption Remy hajaanza mechi yoyote ligini akiwa msimu huu

Meneja wa Aston Villa Remi Garde amesema atajaribu kumchukua nyota wa Chelsea Loic Remy kwa mkopo mwezi Januari.

Garde anataka Mfaransa huyo wa umri wa miaka 28 kutia nguvu timu yake ambayo kwa sasa inashika mkia Ligi ya Premia.

Klabu hiyo imepungukiwa na alama 11 kufikia eneo la kukwepa kushushwa daraja kutoka ligi kuu.

"Loic ni wa kipekee kwa sababu anafahamu taifa hili na ligi hii. Anaweza kufaa sana timu,” Garde amesema.

“Yeye ni mmoja wa wachezaji nitakaotafuta wajiunge na Aston Villa bila shaka."

Garde, ambaye ni Mfaransa pia, alikuwa meneja Lyon Remy alipoanza uchezaji Stade de Gerland.

Meneja huyo wa Villa anatumai mshambuliaji huyo atawasaidia kufunga mabao ambayo yameadimika sana msimu huu.

Villa wamefunga mabao 15 pekee katika mechi 19 ligini, idadi ya chini zadi ligini.

Remy alijiunga na Chelsea kwa£10.5m kutoka QPRmwaka jana.

Ameanza mechi moja pekee Ligi ya Premia msimu huu, na amefunga mabao mawili Kombe la Ligi na moja Ligi ya Premia.