West Ham walaza Liverpool

West Ham Haki miliki ya picha Getty
Image caption West Ham wamelaza mafahali wengi wa EPL msimu huu

Mchezaji wa zamani wa Liverpool Andy Carroll alifungia West Ham na kuwasaidia kulaza klabu hiyo ya Anfield 2-0 mechi iliyochezwa mapema Jumamosi.

Kufuatia ushindi huo, West Ham waliwaruka Liverpool kwenye jedwali na pia wakapata ushindi mechi mbili za ligi msimu mmoja dhidi ya Liverpool mara ya kwanza katika miaka 52.

Michail Antonio alimzidi Nathaniel Clyne na kufikia krosi ya Enner Valencia na kufunga bao la kwanza Ligi ya Premia mwaka 2016.

Carroll, aliyenunuliwa na Liverpool £35m mwaka 2011, alikamilisha ushindi huo baada ya kufikia krosi ya Mark Noble.

Kiungo wa kati wa Liverpool Emre Can aligonga mwamba wa goli lakini vijana hao wa Jurgen Klopp hawawika sana kwenye mechi hiyo.

Ushindi huo wa West Ham umewavusha hadi nambari tano ligini, Liverpool nao wakashuka hadi nambari nane.

Liverpool wamejiunga na Arsenal, Manchester City, Chelsea na Southampton katika kundi la timu ambazo zimecharazwa na West Ham ligini msimu huu.

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp, akizungumza baada ya mechi alisema amekasirishwa sana na matokeo hayo.

“Linalonikasirisha ni kwamba tulipata nafasi ya kucheza mchezo wa kushambulia leo lakini hatukufunga bao hata moja,” alisema Klopp.

“Iwapo unajua kwenye timu ile nyingine kuna Andy Carroll, unakubalije wachezaji wapitishe mipira?"