Chelsea wapata ushindi Crystal Palace

Willian Haki miliki ya picha AP
Image caption Willian alifungia Chelsea bao la pili

Chelsea wamepata ushindi wao wa kwanza chini ya Guus Hiddink na kupanda hadi nambari 14 kwenye jedwali baada ya kulaza Crystal Palace 3-0.

Oscar aliweka Blues kifua mbele dakika ya 29 kabla ya Willian kuongeza la pili dakika ya 60 na Diego Costa kukamilisha ushindi kwa bao dakika ya 66.

Chelsea walionekana kucheza vyema ukilinganisha na mechi za awali, jambo ambalo nahodha John Terry na kiungo wa kati Jon Obi Mikel walikiri baada ya mechi.

Kaimu meneja wao Hiddink, bado hajashindwa mechi hata moja tangu achukue mikoba kutoka kwa Jose Mourinho aliyefutwa kazi mwezi jana.

Hiddink aliwaongoza Chelsea kumaliza nambari tatu Ligi ya Premia, kufika nusufainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na kushinda Kombe la FA kipindi cha kwanza alipokuwa Chelsea.

Mkimbio wa Blues wa mechi nne bila kushindwa ndio mrefu zaidi msimu huu.

Ingawa wamepanda hadi nambari 14 ligini, bado wamepungukiwa na alama 12 kufikia eneo la kufuzu kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Chelsea walikuwa na rekodi mbaya sana ugenini msimu huu na walikuwa wamezoa alama sita pekee nje ya Stamford Bridge.

Ni klabu mbili pekee, Aston Villa na Sunderland, zilizokuwa na rekodi mbaya kushinda hiyo.

Diego Costa, mchezaji ambaye hakuwa akifana kipindi cha kwanza msimu huu, alicheza vyema na kuchangia ufungaji wa mabao yaliyofungwa na wenzake.

John Mikel Obi, aliyechezeshwa badala ya Matic, pia alidhibiti vyema safu ya kati ya Chelsea.

18:21 MECHI INAMALIZIKA Crystal Palace 0-3 Chelsea

Mabao yamefungwa na Oscar 29′, Willian 60′ na Diego Costa 66′.

18:20 Marouane Chamakh anashambulia, lakini anazimwa.

18:18 Palace wanashambulia, Courtois anaudaka mpira na kuurusha upesi kwa Willian anayeshambulia upande ule mwingine. Anajaribu kupenyeza mpira kwa Costa lakini kipa wa Palace yuko macho anauchukua.

18:17 Oscar anaondolewa uwanjani na nafasi yake anaingia Nemanja Matic

18:15 Diego Costa anajaribu kutikisa wavu kwa mpira mkali baada ya kupata mpira kutoka kwa Willian. Anatia nguvu zaidi na mpira unapaa juu ya wavu.

18:11 Jason Puncheon anachezewa vibaya na Fabregas. Anapewa frikiki.

18:09 Costa anaelekea kupata nafasi nzuri ya kufunga. Delaney anachomoka na kutoa mpira nje. Kona inapigwa na mpira unatoka nje.

18:08 Jonny Williams anaingizwa nafasi ya Lee Chung-yong upande wa Palace. Hajachezeshwa kwa kipindi cha miezi 16.

18:08 Diego Costa anachezewa vibaya na Scott Dann na kupata frikiki.

18:05 Zaha anashambulia, John Terry anatoa mpira nje na inakuwa kona. Haizai matunda.

17:58 Palace wanashambulia lakini Courtois anaudaka mpira.

17:58 Lee Chung-yong anajishindia frikiki baada ya kuchezewa vibaya na Mikel.

17:55 Marouane Chamakh anaingia nafasi ya Fraizer Campbell, Joe Ledley naye nafasi ya Mile Jedinak upande wa Palace.

17:54 BAOOO! Crystal palace 0-3 Chelsea

Diego Costa anafungia Chelsea la tatu.

Haki miliki ya picha Getty

17:52 Branislav Ivanovic anapata frikiki.

17:48 BAOOOO! Crystal Palace 0-2 Chelsea

Willian anatoa mpira mkali ambao unatua juu ndani ya wavu. Oscar alikuwa amechezewa vibaya lakini refa akaamua mchezo uendelee.

Haki miliki ya picha Reuters

17:46 Wilfried Zaha anachomoka, anabaki na kipa kati yake na lango lakinia anashindwa kumbwaga. Mambo baco Palace 0-1 Chelsea.

17:40 Chelsea wanapata frikiki baada ya Willian kuchezewa visivyo. Anaipiga. Zouma anaruka juu na kuufikia mpira kwa kichwa lakini anauelekeza juu ya wavu.

17:39 Palace wanashambulia kupita Zaha, lakini Mikel hapitiki.

17:38 Willian anatoa krosi ambayo inazimwa na mpira kutolewa nje. Inakuwa kona anaipiga na inatolewa nje. Anapiga tena lakini Palace wanauondoa hatarini.

17:36 Palace wanaanza kwa kushambulia, Jason Puncheon akitoa krosi kutoka kulia. Lakini mpira huo unadakwa na kipa Thibaut Courtois.

17:35 KIPINDI CHA PILI

17:18 WAKATI WA MAPUMZIKO

Crystal Palace 0 -1 Chelsea

17:17 Jason Puncheon (Crystal Palace) anashambulia lakini mpira wake unakosa goli. Palace wanajaribu tena lakini mpira unatua mikononi mwa Palace.

17:16 Pedro anafanya madhambi.

17:15 Pape Souaré anashinda frikiki.

17:10 Wilfried Zaha wa Palace anajishindia frikiki.

17:05 César Azpilicueta anapata mpira pahala pazuri, anashambulia lakini mpira wake unazimwa na kipa Wayne Hennessey.

17:02 Lee Chung-yong anashambulia lango la Chelsea, lakini mpira wake unapaa juu.

16:59 BAOOOO! Crystal Palace 0-1 Chelsea

Oscar anafungia Chelsea baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Diego Costa.

Haki miliki ya picha Reuters

16:55 Fraizer Campbell wa Palace anashambulia, lakini mpira wake unaelekea nje kulia.

Haki miliki ya picha Getty Images

16:50 Mechi inasimamishwa kwa muda baada ya Joel Ward wa Palace kuonekana kuumia. Baadaye inaendelea.

16:45 Mkwaju wa adhabu unapigwa. Mikel anatoa mpira nje na inakuwa kona ya Palace. Wanashindwa kufunga.

16:44 Pedro anaingia nafasi ya Eden Hazard anayeonekana kuumia.

16:43 Mkwaju wa adhabu dhidi ya Chelsea baada ya John Obi Mikel kucheza visivyo.

16:39 Damien Delaney wa Palace anaonyeshwa kadi ya manjano kwa kumchezea visivyo Diego Costa.

16:38 Chelsea wanapata kona baada ya Mile Jedinak kutoa mpira nje. Haizai matunda.

16:37 Palace waendelea kushambulia Chelsea, Wilfried Zaha akipoteza nafasi nzuri baada ya kupata mpira mzuri kutoka kwa James McArthur.

16:34 Mechi inacheleweshwa kidogo baada ya César Azpilicueta (Chelsea) kuonekana kuumia.

16:30 Crystal Palace 0-0 Chelsea

Palace wanaanza kwa kushambulia na wanapata kona baada ya Zouma kutupa mpira nje. Jason Puncheon anapiga kona hiyo lakini mwishowe mpira unatoka nje.

16:30 MECHI INAANZA

16:29 Hawa hapa ndio wachezaji wa timu zote mbili.

Chelsea

Crystal Palace

16:27 Fabregas na Diego Costa wamerejea kikosini. Costa alikuwa amesimamishwa mechi dhidi ya Manchester United ambayo iliisha 0-0.

Haki miliki ya picha Getty

16:25 Hujambo? Karibu kwa habari za moja kwa moja za Ligi Kuu ya England.

Leo Chelsea wako ugenini Selhurst Park kucheza dhidi ya Crystal Palace wakijaribu kujiinua chini ya meneja mpya Guus Hiddink.