Guardiola asema atahamia Uingereza

Guardiola Haki miliki ya picha All SPort
Image caption Guardiola amesema amekuwa akitaka sana kunoa timu Uingereza

Pep Guardiola amesema kwamba atahama klabu ya Bayern Munich mwisho wa msimu na kwenda kusimamia timu Uingereza.

Meneja huyo wa zamani wa Barcelona amesema hataongeza mkataba wake Ujerumani, utakapomalizika mwisho wa msimu huu.

Guardiola, mwenye umri wa miaka 44, amehusishwa klabu kadha za Uingereza kama vile Manchester City, Manchester United na Arsenal.

"Nataka kupata uzoefu wa mji mpya na nataka kufanya kazi Uingereza,” amesema . "Nimetafutwa na klabu kadha za uingereza lakini zijatatia saini mkataba wowote kwa sasa.’’

Aliongezea kusema "nina fursa ya kufanya kazi Uingereza. Nafikiri niko katika umri sawa na nahisi ni wakati bora kwangu kuhama ni sasa. Hii ndiyo sababu nikachukua uamuzi huu.”

Afisa mkuu mtendaji wa Bayern Munich Karl -Heinz Rummenigge alikuwa amedokeza kwamba Guardiola alikuwa tayari ameamua timu ambayo angejiunga nayo msimu ujao, lakini katika mkutano na wanahabari siku ya Jumanne Guardiola alisema : "Bado sijaamua kuhusu klabu mpya.”

Aliyekuwa meneja wa Real Madrid na Chelsea Carlo Ancelotti, 56, anatarajiwa kuwa meneja mpya wa viongozi hao wa ligi ya Bundesliga.

Guardiola amemtaja Mwitaliano huyo kuwa “chaguo bora”.