Msisimko Tanzania kufuatia ushindi wa Samatta

Huwezi kusikiliza tena

Mashabiki wa soka nchini Tanzania na nyingine za eneo la Afrika Mashariki wamepokea kwa furaha ushindi wa Mtanzania Mbwana Ally Samatta kuwa mchezaji bora wa mwaka anayechezea barani Afrika.

Samatta ni mshambuliaji katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Aliibuka mfungaji mabao bora katika ligi ya klabu bingwa Afrika na kusaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa mwaka jana.

Samatta alibwaga Baghdad Boundjah (Algeria/ Etoile du Sahel) na Robert Kidiaba (DR Congo/ TP Mazembe) kutwaa tuzo hiyo.

Sherehe ya kutangaza washindi wa tuzo hizo zilifanyika mjini Abuja Nigeria usiku. Ingawa habari zilitokea usiku, baadhi ya magazeti yalihakikisha yamechapisha habari za ushindi wake.

Samatta baadaye aliweka kwenye Twitter picha hii inayomuonyesha akiwa na tuzo yake na akiwa amejifunika kwa shiti yenye rangi za bendera ya Tanzania.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Samatta alisema: "Najivunia sana kushinda tuzo muhimu sana kiasi hiki. Naijionea fahari na kuonea fahari taifa langu pia. Natoka taifa (Tanzania) ambalo si moja ya mataifa makubwa katika soka Afrika. Kutawazwa kuwa mchezaji bora Afrika, ni jambo kubwa sana kwangu."