Man City washinda,Chelsea watoka sare

Haki miliki ya picha AFP
Image caption wachezaji wa manchester City wakisherehekea

Mshambuliaji Sergio Aguero alifunga mara mbili na kuisaidia Manchester City kupunguza mwanya wa uongozi wa ligi kuu ya Uingereza kwa kuicharaza Crystal Palace mabao 4-0.

Baada ya kuanza wakiwa chini ,kiungo wa kati Fabian Delph aliwapatia uongozi baada ya kufunga bao safi kutoka mbali.

Mshambuliaji Aguero alifanya mambo kuwa 2-0 baada ya juhudi zilizosababisha mpira kumgonga beki wa Crystal Palace na kuingia wavuni.

Aguero baadaye alimaliza gusa ni guse kwa kucheka na wavu kabla ya David Silva kupata pasi muruwa kutoka kwa Aguero na kufanya mambo kuwa 4-0.

Kufikia sasa Crystal Palace haijashinda katika mechi tano mfululizo.

Kwengineko John Terry alifunga bao lililozua utata katika dakika ya 98 na kuiwezesha Chelsea kupata alama moja dhidi ya Everton.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wachezaji wa Chelsea

Everton walichukua uongozi wakati John Terry alipojifunga huku Ros Barkley wa Everton akipiga chuma cha goli kabla ya Kevin Mirallas kuwaweka kifua mbele wageni na kufanya mambo kuwa 2-0.

Diego Costa alipunguza mwanya huo huku Cesc Fabregas akisawazisha na kufanya mambo kuwa 2-2.

Ramiro Funes Mori aliiweka tena kifua mbele Everton kunako dakika ya 90 kabla ya Terry kusawazisha akiwa karibu na goli licha ya kuonekana kwamba alikuwa ameotea.