Van Gaal: Sijaridhishwa na matokeo yetu

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Van Gaal: Sijaridhishwa na matokeo yetu

Kocha wa Manchester United Louis van Gaal amekiri kuwa matokeo ya timu hiyo hayaridhishi kamwe.

Van Gaal alikiri kuwa walistahili gadhabu ya mashabiki kufuatia msururu wa matokeo duni ambayo kilele chake ilikuwa kichapo cha bao moja kwa nunge dhidi ya Southampton.

Baada ya kichapo hicho Old Trafford, vijana wa Van Gaal walizomewa sana na mashabiki .

Kilichowaaudhi sana ni takwimu kuwa Manchester United ilijifurukuta na kushambulia lango la wapinzani wao mara moja pekee katika mechi hiyo.

Van Gaal alinukuliwa akikiri kuwa yeye pamoja na vijana wake hawakufanya vyema katika mechi hiyo na kuwa walistahili kubezwa na kutupiwa matusi makali na mashabiki.

''Kwa kweli mashabiki hawana kosa lolote kufuatia msururu wa matokeo duni,,,najua kuwa wanamatumaini makubwa na kikosi hiki kwa hivyo

'tunavyoendelea kusajili matokeo yasiyowaridhisha bila shaka watatukemea'.

'Inaniudhi sana kuwa nimeshindwa kuafikia malengo yangu na ya klabu'' alisema mholanzi huyo.

Haki miliki ya picha PA
Image caption 'Inaniudhi sana kuwa nimeshindwa kuafikia malengo yangu na ya klabu'' alisema mholanzi huyo.

United wako katika nafasi ya 5 katika jedwali la ligi kuu ya Uingereza ikiwa na jumla ya alama 37.

Timu hiyo inahitaji zaidi ya alama 5 ilikusalia katika nafasi ya nne za kwanza zitakazoiwezesha kushiriki katika ligi ya mabingwa barani Ulaya mwakani.

Alama hizo 37 ni za chini zaidi katika historia ya klabu hiyo maarufu duniani baada ya kucheza mechi 23.

Wakati kama huu katika msimu uliotangulia United walikuwa na alama tatu zaidi chini ya ukufunzi wake David Moyes.

Manchester United hawajafunga bao lolote katika kipindi cha kwanza katika mechi 11.