Djokovic ambwaga Federer na kutua fainali

Murray Haki miliki ya picha AP
Image caption Djokovic atakutana na mshindi kati ya Andy Murray na Milos Raonic

Novak Djokovic amefuzu kwa fainali ya mashindano ya tenisi ya Australian Open kwa mara ya sita baada ya kumbwaga Roger Federer.

Mchezaji huyo nambari moja duniani amepata ushindi wa 6-1 6-2 3-6 6-3.

Djokovic alitawala seti mbili za kwanza, lakini baada ya muda Federer alianza kujikwamua.

Hata hivyo, Djokovic alifanikiwa kushinda seti ya mwisho.

Hili ni shindano la tatu mtawalia la Grand Slam ambapo Djokovic amemshinda Mswizi huyo ambaye sasa atasubiri kwa muda zaidi kushinda taji lake kuu la 18.

Djokovic atakutana na Mwingereza Andy Murray au raia wa Canada Milos Raonic kwenye fainali.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Djokovic alitawala seti mbili za kwanza

Mserbia huyo amemshinda Murray kwenye fainali mara tatu awali, ikiwa ni pamoja na mwaka jana aliposhinda kwa seti nne.

"Nilicheza vyema sana seti mbili za kwanza lakini ilinibidi kwa sababu Roger amekuwa akicheza vyema sana na nilijua angekuwa mkali,” amesema Djokovic baada ya ushindi wa leo.