Uganda watupwa nje michuano ya Chan

Diarra Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kipa wa Mali Djigui Diarra alisaidia sana kuzuia wasifungwe

Zambia na Mali zimefuzu kwa robo fainali ya michuano ya kombe la taifa bingwa Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani baada ya kutoka sare mechi iliyochezwa Jumatano.

Chipolopolo tayari walikuwa wamefuzu kabla ya mechi hiyo nao Mali walijihakikishia nafasi ya kufuzu kwa kupata alama hiyo moja kwa kutoka sare tasa uwanjani Rubavu.

Katika mechi nyingine ya Kundi D, Zimbabwe walitoka sare na Uganda, baada ya Cranes kusawazisha dakika ya 93.

William Manondo alikuwa ameweka Zimbabwe kifua mbele lakini Geofrey Serunkuma akasawazisha dakika za mwisho.

Uganda walihitaji kuishinda Zimbabwe nao Mali washindwe na Zambia ndipo wapate nafasi ya kufuzu.

Kwenye Kundi hilo, Zambia walimaliza kileleni na alama 7, Mali wa pili na alama 5, Uganda tatu na alama 2 nao Zimbabwe wakashika mkia na alama 1.

Mechi za robofainali zitachezwa Jumamosi na Jumapili, mechi inayosubiriwa sana ikiwa kati ya wenyeji Rwanda na majirani wao DR Congo Jumamosi uwanjani Amahoro.