John Terry kuondoka Chelsea

Terry Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Terry hajapewa mkataba mpya

Nahodha wa Chelsea John Terry anatarajiwa kuondoka klabu hiyo inayocheza Ligi Kuu ya Uingereza mwisho wa msimu huu.

Mkataba wa mchezaji huyo unamalizika mwisho wa msimu na hajapewa mkataba mpya.

Beki huyo wa umri wa miaka 35, aliyejiunga na klabu hiyo akiwa na umri wa miaka 14, ameshinda Ligi ya Premia mara nne, Kombe la FA mara tano na Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara moja akiwa na The Blues.

"Ningependa sana kuendelea kukaa, lakini klabu inaelekea upande tofauti,” amesema.

Terry amechezea Chelsea mara 696 na anatumai kuendelea kucheza, ingawa si katika klabu nyingine Uingereza.

"Walisema kwamba meneja mpya akija, mambo huenda yakabadilika,” Terry alisema baada ya klabu hiyo kulaza MK Dons 5-1 katika raundi ya nne Kombe la FA.

“Kwa sasa sijapata mkataba. Nilitaka kujua sasa kama ilivyokuwa awali kila Januari na hili huchukua miezi kadha kukamilishwa. Hautakuwa mwisho nilioutarajia. Sitastaafu soka nikiwa Chelsea, imechukua siku kadha kukubali hili.”

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Terry alianza kuchezea Chelsea akiwa na miaka 14

Baadaye hata hivyo, msemaji wa klabu alisema huenda Terry akapewa mkataba mpya.

"John ameshauriwa kwamba ingawa kwa sasa hajapewa mkataba wowote, kwamba hali inaweza kubadilika miezi kadha ijayo,” msemaji wa klabu hiyo alisema baadaye Jumapili.

“Klabu hii inamheshimu sana John na kuthamini yote ambayo ametusaidia kutimiza kufikia sasa.”