Denver Broncos washinda Super Bowl

Broncos Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ni mara ya tatu kwa Broncos kushinda SUper Bowl

Denver Broncos wamewazidi nguvu wapinzani wao Carolina Panthers 24-10 na kushinda Super Bowl 50.

Mchuano huo ndio unaosubiriwa kwa hamu zaidi Marekani na ulitazamwa na jumla ya watu 160 milioni kupitia runinga Marekani.

Carolina walipigiwa upatu kushinda, ikizingatiwa kwamba walikuwa wameshindwa mechi moja msimu wote na walikuwa na mchezaji mwenye thamani ya juu zaidi msimu huu Cam Newton.

Lakini Newton alikabwa vilivyo na walinzi wa Broncos.

Broncos walichukua uongozi wa mapema wa 10-0 wakiongozwa na kigogo wao Peyton Manning, na hawakurudi nyuma.

Kulikuwa na uvumi kwamba mechi hiyo ingekuwa ya mwisho kwa Manning, mwenye umri wa miaka 39, lakini alisema baada ya mechi hiyo kwamba atachukua muda kutafakari kabla ya kufanya uamuzi.

Hilo ndilo taji la tatu la Super Bowl kutwaliwa na Broncos, huku Panthers wakiendelea kusubiri kushinda taji hilo kwa mara yao ya kwanza.

Wanamuziki wa Coldplay kutoka Uingereza ndio waliotumbuiza wakati wa mapumziko ambapo waliungana pia na Beyonce, Bruno Mars na Mark Ronson.