Kenya kupata viongozi wapya wa soka

Wajumbe
Image caption Wajumbe 77 kutoka maeneo mbalimbali Kenya watashiriki

Uchaguzi wa kuteua viongozi wapya wa shirikisho la soka la Kenya (FKF) ambao unatarajiwa kurejesha uthabiti katika shirikisho hilo umeanza jijini Nairobi.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya kuahirishwa mara kadha.

Kuna wagombea watano wanaowania wadhifa wa rais wa shirikisho, akiwemo rais wa sasa Sam Nyamweya ambaye ameongoza shirikisho hilo kwa miaka minne sasa.

Wengine ni mwenyekiti wa mabingwa wa ligi Gor Mahia Ambrose Rachier, mwenyekiti wa Kariobangi sharks Nick Mwendwa mfanyibiashara Semi Aina na aliyekuwa naibu mwenyekiti wa soka FKF Sammy Shollei.

Image caption Bw Rachier (Kati) ni mmoja wa wanaowania wadhifa wa urais FKF

Mwandishi wa BBC Abdinoor Aden anasema wajumbe walianza kuwasili asubuhi na mapema uwanjani Kasarani ambako uchaguzi huo unafanyika.

Wajumbe 77 watashiriki kwenye uchaguzi huo.

Uchaguzi huu unatarajiwa kurejesha imani ya Wakenya katika usimamizi wa soka kwani imekuwa ikikumbwa na madai utumizi mbaya wa fedha.

Kenya haijakuwa ikifanya vyema mashindano ya kimataifa. Haikufuzu kwa hatua ya makundi mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2018.

Mwaka uliopita, shutuma zilielekezwa kwa shirika hilo baada ya wachezaji wa timu ya taifa Harambee Stars kuchelewa kusafiri kwenda Cape Verde kwa mechi ya marudio ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi.

Siku chache zilizopita, ripoti zilienea kwenye vyombo vya habari Kenya kwamba viongozi wapya wa muda walikuwa wamesajili na msajili anayehusika na michezo Kenya.

Hatua hiyo ilishutumiwa vikali na Bw Nyamweya aliyeonya kuwa huenda Kenya ikaadhibiwa vikali na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kitendo kama hicho kikifanyika.

Baadaye serikali ilikana kusajili viongozi hao wapya.

Kenya ndiyo itakayokuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Taifa Bingwa Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani mwaka 2018. Michuano ya karibuni iliandaliwa nchini Rwanda ambapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliibuka mabingwa kwa kulaza Mali 3-0 kwenye fainali Jumapili.