Mkuu wa soka Kenya ajiondoa uchaguzini

Nyamweya
Image caption Bw Nyamweya ameongoza FKF kwa miaka minne

Uchaguzi wa viongozi wapya wa shirikisho la soka Kenya (FKF) umechukua mwelekeo mpya baada ya rais anayeondoka Samuel Nyamweya kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wajumbe 77 wanapiga kura kuwachagua viongozi wapya wa shirikisho hilo la kitaifa.

Uchaguzi huo umeahirishwa mara tatu kutokana na sababu ambazo baadhi ya wadau wamesema hazieleweki.

Uongozi wa FKF uligubikwa na utata zaidi baada ya kundi moja lililoongozwa na Gor Semelang’o kujitokeza na kudai kutwaa uongozi wa shirikisho.

Juhudi hizo hazikufua dafu na Bw Semelang’o, ambaye ni mmoja wa wale ambao awali walitangaza nia ya kutaka kumrithi Bw Nyamweya akajiondoa uchaguzini.

Uchaguzi wa leo ulikuwa umevutia wagombea sita wadhifa wa rais wa shirikisho lakini sasa wamesalia wagombea wawili pekee baada ya kujiondoa kwa Bw Nyamweya.

Bw Nyamweya alikuwa ameongoza FKF kwa miaka minne.

Wagombea wengine watatu, Sammy Shollei, Semi Aina na Semelang’o walijiondoa mapema.

Kujiondoa kwa wagombea hao kumeacha kinyang’anyiro sasa kuwa kati ya Nicholas Mwendwa na Ambrose Rachier.