Diego Costa aumia pua mazoezini

Chelsea Haki miliki ya picha Getty
Image caption Chelsea watakutana na Newcastle Jumamosi

Meneja wa Chelsea Guus Hiddink amefichua kwamba mshambuliaji wa klabu hiyo Diego Costa aliumia puani akishiriki mazoezi jana jioni.

Hata hivyo, Mholanzi huyo amesema Costa hayumo hatarini na anatarajiwa kufanya mazoezi madogo leo jioni na kisha kujiunga na wachezaji wenzake hotelini.

Costa anatarajiwa kucheza mechi ya Jumamosi dhidi ya Newcastle.

Hiddink amesema Costa aliumia kimakosa akijaribu kupiga mpira wa kichwa.

Costa hujulikana sana kutokana na utukutu wake uwanjani.

Haki miliki ya picha Getty

Kuhusu beki wa Ufaransa Kurt Zouma, Hiddink amesema mchezaji huyo hataweza kucheza tena msimu huu baada ya kuumia kwenye goti wakati wa mechi dhidi ya Manchester United.

Hata hivyo, amesema klabu hiyo itatumia wachezaji chipukizi kuziba pengo atakaloacha.

"Hatuna wasiwasi wa kuingiza chipukizi,” amesema.

Hiddink amesema klabu hiyo sasa imefanikiwa kuondoa wasiwasi na kutojiamini lakini sasa lazima wachezaji hao waanze kushinda mechi.

Chelsea wametoka sare mechi sita kati ya nane walizocheza tangu Hiddink achukue usukani kufuatia kufutwa kwa Jose Mourinho mwezi Desemba.

Hata hivyo, hawajashindwa mechi hata moja.

"Ingawa ni vyema kutoshindwa, kila mtu sasa anataka tushinde mechi nyingi,” amesema Hiddink.