Voliboli: Cameroon kuvaana na Misri fainali

Cameroon Haki miliki ya picha Guy Suffo CAVB
Image caption Cameroon walishinda Algeria kwa seti 3-0

Cameroon itakutana na Misri kwenye mechi ya fainali leo usiku fainali ya mashindano ya Afrika ya voliboli ya wanawake kufuzu kwa michezo ya Olimpiki.

Kenya, waliobanduliwa na Misri kwa kuchapwa seti 3-2 kwenye nusufainali Jumatatu, watapambana na Algeria kupata mshindi wa tatu.

Cameroon ilishinda Algeria seti 3-0 Jumatatu usiku wiki hii mjini Yaounde mechi hiyo nyingine ya nusufainali.

Algeria ililemewa kabisa na Cameroon ambao walizuia karibu mipira yote ya Algeria huku nyota wa mechi hiyo akiwa Nana Tchoudjang aliyeipatia Cameroon pointi nyingi zaidi, 12, akifuatiwa na Moma Bassoko akiwa na pointi 8. Kwa upande wa Algeria Yasmine Abdelrrahim aliongoza na pointi sita.

Misri nao walihitaji dakika 127 kushinda Kenya kwa seti 3-2 za 25-22, 24-26, 16-15, 25-20 na 19-17.

Wachezaji wa Misri waliochangia pakubwa kwa ushindi huo ni Mariam Metwally na Aya El Shami aliyefunga jumla ya pointi 34, ikiwa ndiyo idadi ya juu zaidi kwenye mashindano haya, naye Nada Meawad akapata pointi 14.

Mashambulizi ya Kenya yalizimwa mara kwa mara na Metwally ambaye alizuia mipira ya wachezaji wa Kenya akiwemo nahodha Mercy Moim, ambaye aliongoza kwa wafungaji akiwa na pointi 19 akifuatiwa na Lydia Maiyo na Joan Chelagat, kila mmoja na pointi 16.

Matokeo yaliyoshangaza wengi ni Botswana kushinda Tunisia seti 3-2 na kuchukua nafasi ya tano. Kwa ushindi huo, mchezaji nyota wa Botswana, Tracy Chaba, anasema wamefurahishwa sana na inaonyesha wana uwezo wa kushinda timu mahiri kama Kenya na Algeria.