Samatta afunga bao la kwanza Ubelgiji

Samatta Haki miliki ya picha Samatta Twitter
Image caption Samatta alisema alifurahia sana kufunga bao

Mshambuliaji nyota wa Tanzania Mbwana Ally Samatta amefungua akaunti yake ya mabao Ulaya baada ya kuifungia klabu yake mpya ya KRC Genk bao dhidi ya Club Brugge.

Samatta alifunga bao lake dakika ya 81 na kusaidia klabu hiyo kupata ushindi wa 3-2 baada ya kuingia uwanjani kama nguvu mpya dakika ya 77.

Klabu yake ilikuwa ikiongoza 2-1 wakati huo.

Club Brugge baadaye waliongeza la pili kupitia mchezaji Vanaken dakika ya 83 lakini hawakufanikiwa kufuta uongozi wa Genk, mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Ubelgiji iliyochezewa uwanja wa nyumbani wa KRC Genk wa Cristal Arena, Jumapili.

Samatta hata hivyo kando na kufunga bao pia alipata kadi ya njano dakika ya 92.

Genk kwa sasa wamo nambari tano ligini wakiwa na alama 45. Club Brugge wanaongoza wakiwa na alama 58.

"Nilikuwa nafikiria kuhusu bao langu la kwanza. Ni vyema kwangu kuanza vyema na timu mpya. Nina furaha sana,” alisema Samatta baada ya mechi hiyo.

"Tumepata ushindi tuliokuwa tukitafuta na ilikuwa muhimu sana.”

Samatta alichezea KRC Genk mechi yake ya kwanza tarehe 6 Februari dhidi ya Moeskroen-Peruwelz, akiingia dakika ya 71. Genk walishinda mechi hiyo 1-0.