Usingizi wamponza mchezaji Ujerumani

Bendtner Haki miliki ya picha Getty
Image caption Bendtner ametozwa faini ya euro 50 kwa kila dakika aliyochelewa

Mshambuliaji wa Wolfsburg Nicklas Bendtner amepigwa faini baada ya kuchelewa kufika mazoezini kwa sababu ya usingizi.

Bendtner, ambaye aliwahi kuichezea Arsenal ya Uingereza, alichelewa kwa dakika 45 baada ya kukosa kusikia mlio wa kengele ya saa ya kumuamsha.

Klabu hiyo imempiga faini ya euro 2,250 (£1,768), euro 50 kwa kila dakika aliyochelewa.

“Sikusikia mlio,” mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Denmark aliambia gazeti la Bild la Ujerumani. “Ni kosa langu”.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 mwezi uliopita pia aliadhibiwa na klabu hiyo baada ya kupakia mtandaoni picha akiwa na gari lake la Mercedes. Sera ya Wolfsburg huwaruhusu wachezaji na wakufunzi kutumia magari ya Volkswagen pekee wakielekea mazoezini.

Aliwahi kupigwa faini ya £80,000 na kupigwa marufuku mechi moja na Uefa baada ya kufichua suruali ya ndani yenye nembo ya mdhamini baada ya kufunga bao dhidi ya Ureno Euro 2012.

Pia alitozwa faini na Arsenal mwaka 2014 kwa kwenda Copenhagen bila idhini.