United washinda debi ya Manchester

Rashford Haki miliki ya picha GETTY
Image caption Rashford alifungia United bao dakika ya 16

Klabu ya Manchester United imeshinda debi ya Manchester iliyochezewa katika uwanja wa Etihad kwa kulaza mahasimu wao City 1-0.

Bao pekee lilifungwa na chipukizi Marcus Rashford dakika ya 16.

Ushindi huo wa United umepunguza mwanya kati ya klabu hizo Ligi ya Uingereza kuwa alama moja pekee.

Aidha, umeongezea United matumaini ya kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

City wamo nambari nne nao United nambari sita.

Katika mechi nyingine, Tottenham Hotspur wamepunguza uongozi wa Leiceter City hadi alama tano baada ya kuilaza Bournemouth 3-0.

Mabao ya Spurs yamefungwa na Harry Kane (1', 16') na Christian Eriksen (52'),

20:54 Mechi inamalizika.

Manchester City 0-1 Mancheter United. Bao pekee lilifungwa na chipukizi Marcus Rashford dakika ya 16.

20:53 Wilfried Bony anamtega Chris Smalling ngome ya United wakati wa shambulio la City.

20:49 Baadhi ya mashabiki wa City wanaanza kuondoka uwanjani.

20:47 Sergio Aguero anapata nafasi lakini anashindwa kufunga.

20:46 Mechi itaongezwa dakika sita. Ni kutokana na muda uliopotezwa baada ya kuumia kwa Joe Hart. Mambo bado ni Manchester City 0-1 Manchester United.

20:45 Tumesalia na dakika chini ya tano.

20:42 Anthony Martial anaanguka eneo la hatari. Refa Michael Oliver anakataa ombi lake la kutaka penalti.

20:40 Dakika ya 82, Matteo Darmian anaonekana kutatizwa na uchovu. Anatolewa uwanjani na nafasi yake anaingia Timothy Fosu-Mensah

20:38 Wilfried Bony anajaribu kugeresha lakini mpira unamchenga.

20:35 Chris Smalling anaponea kuonyeshwa kadi ya pili ya njano. Anamchezea visivyo Sergio Aguero lakini refa anamuonya tu na kutoa mkwaju wa adhabu. Unapigwa na mpira wa kichwa wa Fernandinho anapaa juu.

20:34 Eliaquim Mangala analishwa kadi ya njano kwa kumchezea visivyo Jesse Lingard. Ni dakika ya 75.

20:34 City wanaendelea kushambulia. Mpira wa Jesus Navas unapaa juu.

20:31 Dakika ya 72, David Silva anamuona Sergio Aguero ambaye anautuma mpira kwa Yaya Toure ambaye naye anampitishia Wilfried Bony ambaye anaonekana kutokuwa na bahati kwani mpira wake unazimwa kabla ya kuvuka mstari wa goli.

20:30 Bastian Schweinsteiger anaingia nafasi ya Mhispania Juan Mata.

20:28 City wanazidi kushambulia. Yaya Toure anaukimbiza mpira na kumpa pasi Sergio Aguero, anayembwaga kipa David de Gea kwa kombora, lakini linagonga mlingoti wa goli na kurejea uwanjani.

Haki miliki ya picha EPA

20:27 Antonio Valencia anaingia nafasi ya Marcos Rojo upande wa United.

20:25 David Silva na Sergio Aguero wanashirikiana kushambulia lakini beki kamili wa United Matteo Darmian anazima shambulio lao.

20:20 Sergio Aguero anatuliza mpira kutoka kwa Gael Clichy. Anamshinda mbio Daley Blind na kufika eneo la hatari, lakini kombora lake linapaa juu.

20:11 Martin Demichelis anaondolewa uwanjani na nafasi yake anaingia Wilfried Bony.

20:10 Anthony Martial anamfanyisha kazi Willy Caballero.

20:06 Joe Hart anaondolewa uwanjani akiwa kwenye machela.

20:05 Martin Demichelis anarejesha pasi hafifu kwa kipa wake bila kujua kuna mchezaji nyuma yake. Hart analamika kufanya kazi ya ziada. Anaumia.

20:00 Wachezaji wamerejea uwanjani. Kipindi cha pili kinaanza.

Ni wakati wa mapumzikoManchester City 0-1 Manchester United

19:45 Martin Demichelis anamwangusha Marcus Rashford eneo la hatari. United wanataka penalti lakini, refa anawapuuza.

19:40 Sergio Aguero anamchapa kiatu Daley Blind ambaye anaonekana kuumia. Lakini baada ya muda Blind anainuka na kuendelea na mechi.

19:25 City wanalazimika kubadilisha mchezaji mapema. Raheem Sterling anaonekana kuumia na anatakona na nafasi kuingia Fernando.

Haki miliki ya picha Getty

19:18 Anthony Martial anatoa kombora kali kutoka nje kidogo ya eneo la hatari na kumfanyisha kazi ya ziada kipa wa City Joe Hart.

19:15 BAOOOO!

Marcus Rashford anafungia Manchester United.

Rashford amepokea pasi kutoka kwa Juan Mata, akamchenga Martin Demichelis kisha akambwaga kipa wa City na kutikisa wavu.

Haki miliki ya picha Reuters

19:10 Chris Smalling wa Manchester United anapewa kadi ya njano kwa kumchezea visivyo mshambuliaji wa City Sergio Aguero.

19:07 City wanashambulia. Raheem Sterling anamchenga Matteo Darmian kushoto na kutupa mpira eneo la hatari. Unatulizwa kwa kifua na Jesus Navas anayejipanga na kutoa kombora, lakini linaelekea nje.

Lango la Joe Hart halijashambuliwa kufikia sasa.

19:06 Kumbuka klabu zote mbili zinacheza bila manahodha wake, Vincent Kompany (City) na Wayne Rooney (United) ambao wanauguza majeraha.

19:01 City wanaanza kwa kupata kona. Matteo Darmian analazimika kutupa nje kwa kichwa krosi ya Jesus Navas sekunde ya 20. Kona inapigwa na David Silva lakini haizai matunda.

19:00 Mechi inaanza. Ni debi ya 171 ya Manchester.

18:55 Mameneja wametangaza wachezaji watakaoanza mechi.

United XI: De Gea, Darmian, Smalling, Blind, Rojo, Schneiderlin, Carrick, Lingard, Mata, Martial, Rashford

City XI: Hart, Sagna, Demichelis, Mangala, Clichy, Fernandinho, Toure, Navas, Sterling, Silva, Aguero

18:50 Hujambo! Klabu za jiji la Manchester, Manchester United na Manchester City, zinakabiliana leo katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza. Karibu kwa taarifa za moja kwa moja.

Haki miliki ya picha Reuters