Yanga Azam viwanjani Kombe la Shirikisho

Michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania inaendelea leo kwa michezo miwili katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Azam FC watakua kwenye uwanja wao wa Azam Complex kuwakaribisha maafande wa Tanzania Prisons.

Mabingwa wa Tanzania bara Yanga wao watakua wenyeji wa Ndanda FC katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku kila timu ikihitaji ushindi katika michezo hiyo ili kuweza kufuzu kwa hatua ya nusu fainali.

Aprili 11, Simba SC watakamilisha hatua ya robo fainali kwa kucheza na wagosi wa kaya Coastal Union katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mwadui FC ndio timu pekee mpaka sasa ambayo imeshafuzu kwa hatua ya nusu fainali, baada ya kuwachapa Geita Gold kwa mabao 3 -0.

Bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) atawakilisha Tanzania mwakani kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC) mwaka 2017.