Meneja wa Sunderland asema atahitaji maombi

Sam Haki miliki ya picha PA
Image caption Sunderland wamo nambari 18 ligi ya EPL

Meneja wa Sunderland Sam Allardyce amesema huenda ikambidi kwenda kanisani kufanya maombi baada ya juhudi zake za kusaidia klabu hiyo ya Ligi ya Premia kufana kushindikana.

Hii hasa ni baada ya klabu hiyo kutoka sare tasa na West Brom Jumamosi.

Sunderland walishambulia lango la mara 22, kiwango chao cha juu zaidi msimu huu, lakini walilenga goli mara sita pekee na hawakufanikiwa kufunga.

Hii ilikuwa mara yao ya 10 kushindwa kufunga msimu huu.

“Nahitaji kurudi tena kanisani na kuanza kuomba,”Allardyce aliambia BBC Newcastle.

"Siamini kwamba katika maisha yangu yote kama mkufunzi nimewahi kutawala mechi sana hivyo na nikakosa kushinda.”

Mkufunzi huyo wa miaka 61 aliongeza: “Kawaida, matokeo yangekuwa mbili au tatu bila, iwapo Ben Foster hangekuwa kwenye lango la wapinzani.”

Sare hiyo imewaacha Sunderland nambari 18, alama nne kutoka kwa Norwich walio nambari 17, ambalo ndilo eneo salama.

Hata hivyo wana mechi moja hawajacheza wakilinganishwa na Norwich, ambao watakutana nao Carrow Road tarehe 16 Aprili.

Mechi ijayo ya Sunderland itakuwa dhidi ya viongozi wa ligi Leicester katika uwanja wa Stadium of Light Jumapili.