Mbokani asema hataichezea tena DR Congo

Mbokani Haki miliki ya picha UNIAN
Image caption Mbokani alikuwa uwanja wa ndege wa Zaventem uliposhambuliwa

Mshambuliaji hodari wa timu ya taifa ya DR Congo, Dieu Merci Mbokani amesema hataichezea tena timu ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Hii inafuatia matamshi ya wakuu wa chama cha soka cha nchi hiyo kwamba mshambuliaji huyo lazima achukuliwe hatua kali baada yake kususia mchezo kati ya DR Congo na Angola uliopigwa tarehe 26 Machi jijini Kinshasa.

Mchezaji huyo amesema yeye hakuweza kufika Kinshasa baada ya kunusurika kifo kwenye uwanja wa ndege mjini Brussels alipokuwa wakati wa shambulio la kigaidi dhidi ya uwanja huo.

Dieu Merci Mbokani ambaye pia anaichezea timu ya Norwich ya England, alisema badala ya kumpa pole wakuu wa chama cha soka wamemlaumu kwa kushindwa kuwasili jijini Kinshasa.

Mkuu wa chama cha soka cha Congo Costa Omar ametangaza kwamba lazima Mbokani achukuliwe hatua kali akisisitiza sababu zake za kukataa kwenda Kinshasa hazina msingi.

“Ni bora kupoteza mechi lakini tukiwatumia wachezaji wenye nidhamu,”alisema Costa Omar.

Alitoa mfano wa wachezaji wengine kama Cedric Bakambu, mshambuliaji wa timu ya Villarreal ya daraja la kwanza Uhispania ambaye naye alikuwa ndani ya ndege wakati uwanja wa Brussels ulipovamiwa lakini akabadili uwanja wa ndege na kuwasili mjini Kinshasa.

Katika mechi hiyo Congo iliibamiza Angola 2-1.