Madawa haramu: Wada yaiongezea Kenya muda

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kamati ya kutekeleza kanuni za Wada iliyokutana jana nchini Canada imekubali kuipa Kenya makataa ya hadi Mei tarehe 2 kuhakikisha imepitisha sheria mpya

Shirikisho la kupambana na madawa ya kuongeza nguvu mwilini WADA limeiongezea Kenya muda wa mwezi mmoja zaidi iliihakiki sheria mpya za kumpamaba na kuenea kwa matumizi ya madawa yaliyopigwa marufuku miongoni mwa wanariadha wake.

Kamati ya kutekeleza kanuni za Wada iliyokutana jana nchini Canada imekubali kuipa Kenya makataa ya hadi Mei tarehe 2 kuhakikisha kuwa chama kipya cha kupambana na matumizi ya madawa hayo yaliyopigwa marufuku nchini Kenya NADO na ile halmashauri ya kupambana na madawa hayo haramu ADAK zinapewa msingi wa kisheria.

Hii inafuatia hatua ya bunge la taifa kujadili mara ya kwanza mswada husika.

Kanuni za katiba ya Kenya zinashurutisha mswada ufikishwe bungeni mara mbili na kujadiliwa mara mbili iliipigwe msasa kikamilifu kabla ya kuidhinishwa kuwa sheria.

Inavyoelekea Kenya ilifaulu kuishawishi WADA kuwa hakukuwa na njia nyingine kikatiba ya kuweka sheria hiyo mpya inayolenga kudhibiti matumizi,ununuzi,uuzaji na uzalishaji wa madawa hayo yaliyopigwa marufuku nchini Kenya.

Awali Kenya ilipewa makataa ya hadi mwezi Februati lakini ikashindwa kutekeleza.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Hadi kufikia sasa wanariadha 40 wa Kenya wamepatikana na hatia ya kutumia madawa yaliyopigwa marufuku

Mabingwa hao wa dunia katika riadha waliongezewa muda hadi Aprili tarehe 5 wawe wameweka sheria itakayodhibiti matumizi ya madawa yaliyopigwa marufuku lakini haikuwezekana.

Kenya ilipewa onyo la kupitisha sheria hiyo mpya la sivyo ipigwe marufuku ya kutoshiriki mashindano ya kimataifa baada ya kuenea kwa matumizi ya madawa hayo yaliyopigwa marufuku miongoni mwa wanariadha wake.

Hadi kufikia sasa wanariadha 40 wamepatikana na hatia ya kutumia madawa hayo haramu na kuipaka tope jina la Kenya katika ulimwengu wa riadha.

Kenya ndio mabingwa wa dunia katika riadha .

Wanariadha wakenya wametamba katika mbio tofauti za Marathon kote duniani.

Haki miliki ya picha
Image caption Wanariadha wakenya wametamba katika mbio tofauti za Marathon kote duniani.

Kamati kuu ya WADA itakutana tena tarehe 12 mwezi Mei Montreal Canada kutathmini hatua ambazo Kenya itakuwa imetekeleza kuhakikisha sheria hiyo mpya imepewa msingi wa kikatiba.

Iwapo kufikia siku hiyo Kenya haitakuwa imepisha sheria hiyo basi kamati hiyo haitakuwa na budi ila kuiratibu Kenya kama mataifa ambayo yanahujumu vita dhidi ya matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini.