Moyes ataka kupewa kazi Aston Villa

Moyes Haki miliki ya picha PA
Image caption Moyes alifutwa na Real Sociedad mwishoni mwa mwaka jana

Meneja wa zamani wa Manchester United David Moyes anataka kuwa meneja wa klabu iliyoshushwa daraja ya Aston Villa.

Hata hivyo, klabu hiyo bado haijawasiliana naye.

Ni karibu miezi sita tangu mkufunzi huyo apigwe karamu na klabu ya Real Sociedad ya Uhispania.

Moyes amesema anataka sana kurejea katika ulingo wa soka na kwamba anafurahishwa na kazi ya kufufua Villa.

Raia huyo wa Scotland mwenye umri wa miaka 52 alitazama mechi ya Aston Villa moja kwa moja majuzi na amesema anaweza kukubali ombi la kuwa mkufunzi wao.

Hata hivyo, amesema anafahamu kwamba kunaweza kuwa na changamoto kutokana na bajeti ndogo ya klabu hiyo msimu ujao.

Moyes alikuwa mkufunzi wa Everton kwa muda mrefu kabla ya kwenda kumrithi Sir Alex Ferguson klabu ya Manchester United.

Alifutwa kazi kabla ya kumaliza msimu mmoja.

Nigel Pearson bado ndiye anayepigiwa upatu kuchukua kazi hiyo.

Meneja huyo wa zamani wa Leicester City hajapata kazi tangu aondoke klabu hiyo Juni mwaka jana.

Mameneja wengine ni Mick McCarthy, Sean Dyche na Steve Bruce, ambao kwa sasa ni wakufunzi wa Ipswich, Burnley na Hull City mtawalia.