Mtibwa sugar wako tayari

Kuelekea mchezo ujao wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Mtibwa Sugar, uliopangwa kuchezwa tarehe 30 mwezi huu kwenye uwanja wa Manungu Complex uliopo Turiani mkoani Morogoro, Mkuu wa kitengo cha utabibu kwenye kikosi cha Mbeya City Fc, Dr Joshua Kaseko amesema vijana wake wote wako tayari kwa vita hiyo ya mwisho wa mwezi.

Akizungumza na mbeyacityfc.com mapema wiki hii wakati wa mazoezi ya kikosi hicho kwenye uwanja wa shule ya sekondari Igawilo,Dr Kaseko aliweka wazi kuwa kurejea kwa mlinzi Deo Julius aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu umetia moyo licha ya matizamio ya siku kadhaa kabla ya kumkabidhi rasmi kwa kocha Kinnah Phiri kuendelea na program za mazoezi.

Sina majeruhi kwenye kikosi changu, Deo Julius aliyekuwa kwenye majeruhi ya muda mrefu tayari anarudi kikosini, tuko kwenye matazamio ya mwisho kabla ya kumkabidhi kwa kocha mkuu kuendelea na program za mazoezi,tulipata pointi tatu mchezo uliopita baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo, hili limetuongezea nguvu na sasa morali ni kubwa kuelekea mchezo huo. Kuhusu nafasi kwenye msimamo wa ligi Dr Kaseko alisema kuwa licha ya City kuwa kwenye nafasi ya 10 hivi sasa kwenye msimamo wa ligi lakini hana shaka timu yake aitakuwa sehemu ya vikosi 16 vya msimu ujao wa ligi kuu ya vodacom Tanzania Bara.

''Ndiyo, tuko kwenye nafasi 10 hivi sasa lakini nikutoe wasiwasi tu kuwa timu yetu itakuwa sehemu ya timu 16 za ligi msimu ujao, hatuna shaka kwa sababu baada ya michezo ya mzunguko ujao msimamo wa ligi utatuonyesha tuko kwenye nafasi ya nane, hivyo kwa namna yoyote sisi hatufikirii kuhusu kutokuwepo msimu ujao''.