Kenya yakaribia kutimiza masharti ya Wada

Olimpiki Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kenya ilikabiliwa na hatari ya kuzuiwa kushiriki michezo ya Olimpiki mjini Rio

Kenya imekaribia kutimiza masharti ya shirika la kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli duniani, WADA, baada ya Bunge la nchi hiyo kupitisha mswada wa kukabiliana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku kwenye michezo.

Shirika hilo lilikuwa limeipa Kenya makataa mapya ya hadi Mei 2 kuidhinisha sheria hiyo la sivyo ikabiliwe na hatari ya kuadhibiwa.

Mswada huo mpya unaharamisha matumizi ya dawa za kusisimua misuli na kuweka mikakati ya kukabiliana na wanaohusika.

Wanariadha karibu 40 wameadhibiwa na Shirika la Riadha Duniani (IAAF) kwa kupatikana wakiwa wametumia dawa hizo tangu mwaka 2012.

Mwanariadha mashuhuri Rita Jeptoo, aliyeshinda mbio za marathon za Boston mara tatu na Chicago pia ni miongoni mwa walioadhibiwa.

Waziri wa michezo Hassan Wario alisema kupitishwa kwa mswada huo ni hatua muhimu katika kutimiza masharti ya Wada.

Masharti hayo yalikuwa ni pamoja na kupitishwa kwa sheria ya kudhibiti matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwili, pamoja na kutolewa kwa ufadhili wa kila mwaka wa $50,000 milioni kwa idara ya kukabiliana na tatizo hilo.

Huwezi kusikiliza tena

Alisema Rais Uhuru Kenyatta ataidhinisha mswada huo kuwa sheria karibuni.

Bw Kenyatta, akizungumza wiki iliyopita, alisema bila shaka ataidhinisha sheria hiyo kuhakikisha Kenya haifungiwi nje ya Michezo ya Olimpiki ya Rio ambayo itafanyika kuanzia Agosti 5 hadi 21.

Afisa mkuu wa mawasiliano wa Bunge la Kenya Martin Mutua aliambia shirika la habari la Reuters kwamba kifungu muhimu zaidi ni nambari 29 kinachoangazia kukamatwa na kushtakiwa kwa wahusika.

"Jukumu la kuwakamata na kuwafungulia mashtaka watu wanaohusika katika matumizi ya dawa za kutitimua misuli litakuwa chini ya Mkuu wa Polisi na si maafisa wanaofuatilia utimizwaji wa masharti kama ilivyokusudiwa awali. Kama taifa huru, hatuwezi kuruhusu mawakala wasimamia jambo hili muhimu,” alisema.

Tatizo la dawa zilizoharamishwa kwenye riadha Kenya

  • Kufikia 2011, zaidi ya wanariadha 40 walikuwa wamepatikana wametumia dawa za kuongeza nguvu mwilini.
  • Kufikia Januari 2016, wanariadha 18 wa Kenya walikuwa wanatumikia marufuku
  • Wanariadha hao 18 walikuwa wanatumikia marufuku ya jumla ya miaka 55
  • Maarufu zaidi ni Rita Jeptoo, mshindi wa marathon za Boston na Chicago
  • Lilian Moraa Mariita anatumikia marufuku ndefu zaidi – miaka minane.