Infantino: Video zitawasaidia waamuzi Kombe la Dunia

Infantino Haki miliki ya picha AP
Image caption Infantino amesema majaribio yataanza karibuni

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino ameeleza matumaini yake kwamba michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 itakayofanyika nchini Urusi, itakuwa ya kwanza kutumia msaada wa picha za video kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi kufanya uamuzi sahihi.

Mwezi Machi mwaka huu, Bodi ya Kimataifa ya mchezo huo (IFAB) ilisema kuwa itafanyia majaribio teknolojia hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ili kusaidia kuamua mabao yanayofungwa, kadi nyekundu, makosa ya kufananisha na penalti.

IFAB ilikuwa imepanga kuanza kufanya majaribio hayo msimu wa 2017-2018 lakini Infantino amesema majaribio yataanza sasa na kuchukua muda wa miaka miwili.

Infantino raia wa Uswizi ambaye alichukua nafasi ya Sepp Blatter Februari mwaka huu aliongeza kuwa mpaka kufikiza Machi 2018 watakuwa wamehafahamu kama mfumo huo utafaa au haufai.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) limeichagua kampuni ya Uingereza ya Hawk-Eye kutumika katika mechi zote za michuano ya Euro 2016.

Mfumo wa Hawk-Eye ambao ndio unaotumika katika mechi za Ligi Kuu ulichaguliwa badala ya ule wa kampuni ya Ujerumani wa Goal Control ambao ulitumika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.