Nyota wa Leicester akubali mashtaka ya FA

Vardy Haki miliki ya picha AP
Image caption Vardy alimkaripia refa Jon Moss

Mshambuliaji wa viongozi wa Ligi Kuu ya Uingereza Leicester Jamie Vardy amekubali mashtaka ya utovu wa nidhamu.

Mchezaji huyo wa umri wa miaka 29 alimkaripia mwamuzi Jon Moss baada ya kufukuzwa uwanjani wakati wa mechi ya Jumapili ambayo walitoka sare 2-2 na West Ham.

Kwa kukubali shtaka hilo la Shirikisho la Soka la Uingereza (FA), Vardy, ambaye alikuwa ameitisha kikao cha kujitetea, huenda akaongezewa adhabu juu ya adhabu ya sasa ya kutoruhusiwa kucheza mchezo mmoja.

Klabu ya Leicester pia imekiri shtaka la kukosa kudhibiti wachezaji wake wakati wa mechi hiyo.

Vardy, anayeongoza kwa ufungaji mabao ligini, akiwa na mabao 22, atakosa mechi yao ya Jumapili dhidi ya Swansea na akiongezewa adhabu huenda basi akakosa mechi dhidi ya Manchester United tarehe 1 Mei.

Leicester, wamo alama tano mbele ya Tottenham, na wanahitaji alama nane kutoka kwa mechi zao nne zilizosalia ili kutwaa taji.

Mechi zao nne za mwisho ni dhidi ya Swansea (nyumbani), Manchester United (ugenini), Everton (nyumbani) na Chelsea (ugenini).