Vardy kukosa mechi muhimu dhidi ya Man Utd

Vardy Haki miliki ya picha AP
Image caption Vardy alimkaripia refa Jon Moss

Mshambuliaji wa Uingereza Jamie Vardy atakosa mechi ya klabu yake Leicester City dhidi ya Manchester United Jumapili baada ya kuongezewa adhabu kutokana na utovu wa nidhamu.

Ameongezewa marufuku ya kutocheza mechi nyingine baada yake kukisi kosa la utovu wa nidhamu.

Vardy alimkaripia mwamuzi wa mechi Jon Moss baada yake kuoneshwa kadi nyekundi wakati wa mechi yao dhidi ya West Ham tarehe 17 Aprili ambayo iliisha sare ya 2-.

Leicester huenda wakatwaa taji la Ligi ya Premia iwapo watashinda mechi hiyo itakayochezewa Old Trafford baada ya Spurs kutoka sare 1-1 na West Brom.

Baada ya kukosa mechi ya Jumapili ambayo Leicester walishinda 4-0 dhidi ya Swansea, Vardy sasa pia atakosa uhondo wa siku hiyo iwapo watashinda.

Mchezaji huyo wa miaka 29 pia amepigwa faini ya £10,000.

Vardy atakuwa huru kucheza mechi mbili za mwisho msimu huu dhidi ya Everton (nyumbani) na Chelsea (ugenini), ambapo Leicester watakuwa na nafasi zaidi ya kushinda taji iwapo watashindwa kulaza Manchester United Jumapili.