Cristiano Ronaldo kukabili Man City Uefa

Ronaldo Haki miliki ya picha AP
Image caption Ronaldo amefunga mabao 93 Ulaya

Mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo yuko sawa kuchezea klabu yake dhidi ya Manchester City katika mechi ya nusufainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Mechi hiyo ya marudiano itachezewa Santiago Bernabéu kuanzia saa nne kasorobo usiku. Mechi ya kwanza ilimalizika 0-0.

Ronaldo, ambaye amefunga mabao 93 mechi za Ulaya, hakuweza kucheza mechi ya mkondo wa kwanza kutokana na jeraha misuli ya paja.

"Cristiano yuko sawa, 100%. Alishiriki mazoezi leo na atakuwepo kesho,” meneja wa Real Zinedine Zidane alisema Jumanne.

Kiungo wa kati wa City Yaya Toure, ambaye pia alikosa mechi ya kwanza kutokana na jeraha alifanya mazoezi Jumanne pia.

Kiungo wa kati Samir Nasri, mshambuliaji David Silva na beki Pablo Zabaleta wote hawatarajiwi kuchezea City.

Meneja wa Manchester City Manuel Pellegrini amewatahadharisha wachezaji wake kumhusu Ronaldo.

"Cristiano daima atasalia kuwa mchezaji tofauti. Hufunga mabao mengi na amekuwa akifanya hivyo miaka yote sita ambayo amekuwa hapa,” amesema Mchile huyo aliyekuwa mkufunzi wa Real klabu hiyo ilipomnunua Ronaldo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Pellegrini anaamini Aguero atawatatiza walinzi wa Real

Lakini ameongeza kusema: "Sidhani Real ni Cristiano Ronaldo pekee. Lazima tufanye bidii kama timu kujilinda na kushambulia. Sio dhidi ya Ronaldo pekee lakini dhidi ya Real Madrid."

Amesisitiza pia kwamba klabu hiyo ya Uhispania pia itakuwa na kibarua kudhibiti washambuliaji wa City, akimtaja Sergio Aguero aliyefunga mabao 28.

Aguero alipumzishwa mechi ambayo City walilazwa 4-2 ugenini Southampton Jumapili.

Upande wa Real, bado kuna shaka kumhusu Karim Benzema.

Kiungo wa kati wa Brazil Casemiro aliumia kidogo wakati wa mechi ya La Liga Jumamosi ambayo walishinda 1-0 ugenini Real Sociedad lakini anatarajiwa kukabili City.

Mshinid atakutana na Atletico Madrid kwenye fainali 28 Mei mjini Milan. Atletico waliwaondoa Bayern Munich nusu fainali.