Kipa wa Cameroon aaga dunia

Image caption Jeanine Christelle Djomnang
Kipa wa timu ya taifa ya Cameroon upande wa wanawake ameaga dunia baada ya kuzirai wakati wa mazoezi, Shirikisho la soka la Cameroon limesema.Jeanine Christelle Djomnang,mwenye umri wa miaka 26, aliuguwa kabla ya mechi ya Femina Stars Ebolowa kusini mwa Cameroon Jumapili na alifariki akipelekwa hospitalini.

Shirikisho hilo linasema taarifa za awali zinaashiria alikufa kutokanana mshtuko wa moyo lakini sasa linasubiri taarifa rasmi ya madaktari.

Kifo chake kinajiri baada ya mchezaji wa Cameroon Patrick Ekeng kufariki Romania.

Djomnang alilalamika kuhisi uchungu kifuani alipokuwa akijitayarisha kwa mechi dhidi ya Louves MINPROFF Yaounde na alikimbizwa hospitali.

Mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora mwanamke Afrika raia wa Cameroon Gaelle Enganamouit, ambaye sasa anachezea timu ya Sweden, ni mojawapo ya watu wa kwanza kussikitishwa na habari hizo.

"Ni kwa huzuni mwingi nimepata kusikia kuhusu kifo cha mchezaji mwenzangu Djomnang Jeanine Christelle wa Femina Stars Ebolowa, Mungu ailaze roho yake kwa amani," aliandika katika mtandao wa kijamii.

Kitabu cha rambi rambi kimewekwa katika makao makuu ya shirikisho la soka Cameroon kumkumbuka Ekeng na Djomanang.