West Ham walaza Manchester United

West Ham Haki miliki ya picha GETTY
Image caption West Ham walishinda 3-2

Klabu ya West Ham United iliaga uwanja wake wa nyumbani wa Upton Park kwa kuvuruga juhudi za Manchester United za kutaka kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumanne.

Ilikuwa mechi ya mwisho kuchezewa uwanja huo ambao umetumiwa na West Ham kwa miaka 112 kabla ya kuhamia uwanja wa Olimpiki.

Kwenye mechi hiyo ya kusisimua, West Ham walichomoza na ushindi wa 3-2.

Vurugu zilitokea kabla ya mechi.

Vijana wa Louis van Gaal walifahamu kwamba ushindi dhidi ya klabu hiyo na baadaye ushindi dhidi ya Bournemouth vingewahakikishia nafasi katika ligi kuu ya klabu Ulaya.

Lakini kushindwa kwao kuna maana kwamba Manchester City, walio nambari nne, wamo alama nne mbele yao kabla yao kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Swansea City.

West Ham walitangulia kupitia bao la Diafra Sakho kipindi cha kwanza, lakini Antony Martial aliwasawazishia Red Devils kwa bao dakika ya 51 na kisha akawaweka kifua mbele dakika ya 72.

West Ham, hata hivyo, walijikwamua kwa kufunga mabao mawili ya kichwa katika kipindi cha dakika nne kupitia Michail Antonio na Winston Reid.

Haki miliki ya picha Reuters

West Ham bado wana nafasi ya kumaliza katika nambari tano.

Wamo alama moja nyuma ya Manchester United na watazuru Stoke Jumapili.

Manchester United, watakuwa wenyeji wa Bournemouth, mechi ambayo watahitajika kushinda kujiimarishia uwezekano wa kumaliza katika nne bora.