Serengeti Boys wawasili India

Serengeti
Image caption Vijana hao watakutana na Marekani Mei 15

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Tanzania maarufu kama Serengeti Boys imetua jijini Goa, India kwa ajili michuano maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIFF).

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza leo Mei 12, 2016 kwa mfumo wa ligi kwa timu tano kucheza mechi nne, Tanzania itafungua dimba dhidi ya Marekani kwenye Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia Mei 15, mwaka huu.

Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malaysia Mei 21.

Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utachezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa nchini India.

AIFF kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.