Chelsea na Tottenham wapigwa faini kubwa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Chelsea dhidi ya Tottenham

Chelsea na Tottenham wamepigwa faini kutokana na mashtaka matatu ya kushindwa kuwadhibiti wachezaji wao katika sare ya 2-2 katika uwanja wa Stamford Bridge.

Chelsea watalazimika kulipa pauni 375,000 baada ya kukiuka sheria za shirikisho la soka nchini Uingereza kuhusu makabiliano ya wengi ikiwa ni mara ya nne tangu mwezi Novemba 2014.

Spurs wamepigwa faini ya pauni 225,000 ikiwa ni kisa chao cha tatu kutokea.Mechi hiyo ilikuwa na kadi 12 za manjano .

Mapema mwezi huu mchezaji wa Spurs Mousa Dembele alipigwa marufuku kwa mechi sita kutokana na ghasia katika mechi hiyo hiyo ambayo ambayo ilimaliza matumaini ya Tottenham kushinda ligi ya Uingereza.

Kiungo wa kati wa Ubelgiji Dembele mwenye umri wa miaka 28 alionekana akimgusa jicho mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa.

Mkufunzi wa Tottenham Mauricio Pochettino aliingia uwanjani ili kuwatawanya mlinzi wa Spurs Danny Rose na mshambuliaji wa Chelsea Willian na mwisho wa mechi, Rose alihusika tena na makabiliano yaliomuhusisha kocha wa Blues ambaye alisukumwa na kuanguka sakafuni.