Rashford kusalia Man United hadi 2020

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rashford kusalia Man United hadi 2020

Mshambulizi chipukizi wa Manchester United Marcus Rashford ametia sahihi mkataba mpya utakaohakikisha anasalia Old Trafford hadi Juni 2020.

Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 18 amekonga nyoyo za wafuasi wa Manchester United tangu alipoisaidia timu yake kuizaba Midtjylland katika mechi yake ya kwanza mwezi Februari.

Rashford ameichezea Man United katika mechi 18 na kuifungia mabao 8.

Rashford amejiunga na timu ya England itakayoshiriki katika michuano ya Euro 2016.

Ijumaa iliyopita talanta yake ilingaa zaidi alipofuma bao la kwanza la kimataifa dhidi ya Australia.

Image caption Kijana huyo anakisiwa kuwa analipwa takriban pauni £20,000 kwa Juma.

"Ama kweli ninafuraha sana kuwa nilipewa fursa ya kunadi talanta yangu '' alisema Rashford.

Kijana huyo anakisiwa kuwa analipwa takriban pauni £20,000 kwa Juma.

Naibu mwenyekiti wa Manchester United bwana Ed Woodward alimmiminia sifa kedekede chipukizi huyo

''bado ni kijana sana huyo kwa hivyo tunahitaji kumpa muda zaidi iliakomae kitaaluma , kwa sasa tunashuhudia akinoa makali yake na bila shaka atakuwa mchezaji nyota katika siku za usoni''

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kandarasi hizo zimetangazwa siku 3 tu baada ya kutangazwa kwa kocha mpya Jose Mourinho

Mlinzi Cameron Borthwick-Jackson, 19, ambaye pia alikuwa amesalia na mwaka mmoja kwenye kandarasi yake pia alitia sahihi kandarasi mpya itakayomweka Old Trafford hadi mwaka wa 2020.

Kandarasi hizo zimetangazwa siku 3 tu baada ya kutangazwa kwa kocha mpya Jose Mourinho atakayehudumu Old Trafford kwa kipindi cha miaka mitatu.

Rashford aliwakilishwa na Chris na Wayne Welbeck, ndugu za Danny,anayeichezea klabu pinzani ya Arsenal.