Historia ya Arsenal

Mwanzo hadi Vita ya Kwanza ya Dunia

Maisha ya klabu ya soka ya Arsenal yalianza pale kikundi cha wafanyakazi katika kiwanda cha kuzalisha zana za kivita cha Woolwich walipoamua kuunda klabu ya soka mwishoni mwa mwaka 1886. Klabu ikawa ikishiriki michezo huku ikijulikana kama Dial Square. Mchezo wao wa kwanza waliifunga timu ya Eastern Wanderers 6-0, tarehe 11 Desemba 1886.

Baada ya muda mfupi, jina likabadilishwa na kuwa Royal Arsenal huku timu ikiendelea kushiriki katika michezo ya kirafiki na mashindano ya nyumbani kwa kipindi cha miaka michache iliyofuata.

Mwaka 1891 klabu ikawa ya kulipwa na kubadilisha jina na kuitwa Woolwich Arsenal na hatimaye kujiunga na ligi ya soka mwaka 1893. ‘Washika bunduki’ hao wakahamia Highbury mwaka 1913 kama timu ya ligi daraja la pili. Baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia, Arsenal wakapigiwa kura na kuingizwa katika ligi daraja la kwanza, iliyokuwa imeongezwa ukubwa, ambako wameendelea kudumu hadi leo.

Chapman na kipindi cha mafanikio miaka ya 1930

Herbert Chapman alichukua nafasi ya kuiongoza Arsenal mwaka 1925, na mwaka 1930 akaiwezesha kupata taji lao la kwanza kabisa pale walipoifunga Huddersield katika fainali ya kombe la FA. Mwaka uliofuata Arsenal wakawa mabingwa kwa mara ya kwanza. Kati ya mwaka 1933 na 1935 timu ikaweza kunyakua ubingwa mara tatu mfululizo (hali ambayo imeweza kufikiwa tu na timu nne vigogo). Chapman alifariki katikati ya safari hiyo ya mafanikio akiwa tayari ni mtu wa historia kubwa klabuni.

George Allison alichukua jukumu la kuiongoza Arsenal na timu ikaendelea kufanya vyema katika kipindi kilichobaki katika muongo huo. Ikashinda taji moja zaidi la FA (1936) na taji jingine (1938). Katika kipindi hiki Arsenal ilikuwa na wachezaji mahiri kama vile Alex James, Ted Drake, Cliff Bastin, David Jack, Eddie Hapgood na George Male na wengine ambao wanatajwa kama miongoni mwa wachezaji mahiri kuweza kucheza ligi hiyo.

Baada ya vita na vikombe viwili

Vita ya Pili ya Dunia ilikata mwendo kasi wa Arsenal. Lakini baada ya vita hivyo Tom Whittaker akawa meneja na mafanikio zaidi yakafuata. Arsenal wakawa mabingwa 1947/48 na 1952/53; washindi wa kombe la FA 1950 na washindi wa pili 1952. Miaka ya 1960 haikuwa ya mng’ao kwa Arsenal. Wakapoteza mechi za fainali katika kombe la ligi 1968 na 1969 ikiwa ndiyo hatua pekee kubwa waliyoweza kufikia.

Bertie Mee alikuwa amechukua jukumu kama meneja katikati ya miaka ya 1960 na Arsenal wakanyakua kwa mara ya kwanza kombe la ubingwa la Ulaya mwaka 1969/70 kwa kuifunga Anderlecht 4-3 katika mechi mbili za fainali ya kombe la Fairs.

Mambo mazuri yalikuwa mbioni kujiri kwa mwaka uliofuata. Kikosi cha Arsenal kikiwa na wachezaji kama Charlie George, George Armstrong, Ray Kennedy na nahodha Frank McLintock kilishinda ligi na kombe la FA. Walinyakua taji la ligi katika uwanja wa White Hart Lane kisha wakaifunga Liverpool baada ya muda wa ziada katika uwanja wa Wembley na kunyakua kombe la FA.

Kikosi hicho kikarudi tena Wembley kwa kucheza fainali tatu mfululizo za FA chini ya Terry Neill mwishoni mwa muwongo huo, ambapo walishinda fainali ya pili kati ya hizo tatu kwa kuibanjua Manchester United 3-2. Mchezo huo ukaja kujulikana kama Fainali ya Dakika Tano (Five Minute Final).

Washika bunduki pia wakafika fainali ya kombe la washindi, kikosi kikiwa na wachezaji kama Graham Rix, Frank Stapleton, Pat Rice, David O’Leary na Liam Brady lakini wakapoteza mchezo kwa Valencia.

Heshima ya George Graham

Mwaka 1986 George Graham, aliyekuwa mchezaji katika kikosi kilichochukua ubingwa 1971, akawa meneja akichukua nafasi ya Don Howe. Siku njema zaidi zikafuata. Akaiongoza Arsenal kunyakua kwa mara ya kwanza kombe la ligi mwaka 1986/87 kwa kuifunga Liverpool katika fainali.

Miaka miwili baadae washika bunduki wakanyakua ubingwa wa ligi na goli maarufu la dakika ya mwisho kutoka kwa Michael Thomas na matokeo kuwa 2-0 ndani ya Anfield. Taji jingine ikawa mwaka 1990/91 wakiwa na kikosi kilichopoteza mchezo mmoja tu wakijivunia ukuta imara wa mabeki wanne.

Vikombe zaidi vikafuata. Mwaka 1992/93 Arsenal ikawa klabu ya kwanza kuchukua vikombe vyote vya ligi ya England katika msimu mmoja. Sheffield Wednesday ndiyo timu iliyokumbana na zahama la Arsenal katika matukio yote yote mawili. Kipindi cha mafanikio cha meneja Graham kiling’ara zaidi msimu uliofuata.

Mbio za mafanikio katika Kombe la Washindi la Ulaya zikafika tamati kwa Arsenal kuichapa Parma 1-0 katika fainali jijini Copenhagen kwa bao la Alan Smith. Msimu uliofuata Arsenal wakashindwa kulibakiza kombe mbele ya Real Zaragoza mwaka 1995. Katika wakati huu George Graham alikuwa ameondoka Arsenal. Nafasi yake ikarithiwa na Bruce Rioch ambaye alikamata umeneja kwa msimu mmoja na ndiye aliyefanikisha kusajiliwa Dennis Bergkamp.

Wakati wa Arsene Wenger

Msimu kamili wa kwanza wa Arsene Wenger 1997/98 katika uwanja wa Highbury, ulishuhudia Arsenal kwa mara ya pili katika historia yake ikifanikiwa kunyakua vikombe vyote viwili; cha Ligi Kuu na FA na kumwezesha mfaransa huyo kuchukua tuzo ya Carling ya meneja bora wa mwaka.

Dennis Bergkamp akawa mwanasoka bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Soka (FWA) na mwanasoka bora wa mwaka wa Chama Cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA). Msimu huo uling’ara zaidi kwa wanasoka wa Arsenal kutoka kifaransa Emmanuel Petit na Patrick Vieira baada ya kutoa mchango wao mkubwa katika ushindi wa timu yao ya taifa katika fainali za kombe la Dunia 1998.

Arsenal kwa miaka mitatu mfululizo ikakamata nafasi ya pili na mwaka 2000 ikafika fainali ya kombe la UEFA na kupoteza mchezo. Mwaka 2001, Arsenal ikafika robo fainali ya Kombe la Mabingwa wa Ulaya kabla ya kutolewa na Valencia.

Kipindi cha 2001/02 mambo yakawa mazuri pale walipoweza tena kuchukua vikombe vyote viwili kwa kuichapa Chelsea katika fainali ya FA na kubeba kombe la ligi kwa kuilaza Manchester 1-0 katika mechi kali ya kukumbukwa katika uwanja wa Old Trafford na kufikisha rekodi ya michezo 13 bila ya kufungwa. Katika msimu mzima huo hawakuwahi kufungwa nyumbani. Hivyo Arsenal Wenger akatajwa meneja bora wa mwaka wa Barclays na Robert Piles akatajwa kuwa mwanasoka bora wa Chama cha Waandishi wa habari za michezo (FWA).

Msimu uliofuata Arsenal wakashindwa kwa ufinyu kubakisha kombe lakini wakaweza kuwa kuwa klabu ya kwanza kwa zaidi ya miaka 20 kuweza kubakisha kombe la FA baada ya kuilaza Southampton 1-0 uwanjani Cardiff. Thierry Henry akachaguliwa na PFA na FWA kuwa mchezaji bora wa mwaka. Henry akawa ameweza kujiunga na Bergkamp katika orodha ya wachezaji walioweza kuifungia Arsenal magoli 100.

Kutopoteza mechi msimu mzima

Msimu wa 2003/04 Arsenal wakamaliza michezo yote bila ya kufungwa na kuchukua taji la ubingwa ligi. Pia walimaliza michezo yote wakiwa pointi 11 mbele ya mshindi wa pili Chelsea na kubeba taji kwa mara ya 13. Wakati huo huo Cesc Fabregas ambaye aliwasili Arsenal mwezi wa kwanza, akaweza kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo kabisa kuchezea Arsenal akiwa na umri wa miaka 16 na siku 177 wakati msimu unamalizika.

Vipigo vya nusu fainali ya FA walivyovipata kutoka kwa Manchester United na robo fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya toka kwa Chelsea vikaondoa matumaini yote ya kunyakua vikombe vitatu. Rekodi ya kutofungwa ikaendelea msimu uliofuata na mwezi wa nane Arsenal ikaipiku rekodi ya Nottingham Forest ya kucheza muda mrefu bila ya kufungwa katika ligi ya England.

Washika bunduki wakawa wamejipatia mataji matano katika misimu mine baada ya kuchukua kombe la FA kwa ushindi wa penati dhidi ya Manchester United.

Kampeni ya 2005/06 ilikuwa ya mwisho katika uwanja wa Highbury ambao ulikuwa ni makazi ya Arsenal kwa miaka 93. Timu ikaweza kukamata nafasi ya nne mwisho wa msimu na kuweza kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa wakati wote ilipokuwa Highbury, rekodi ya Arsenal ni kama ifuatavyo: Michezo 2,010; kushinda 1,196; sare 475; shindwa 339; magoli 4, 038; goli za kufungwa 1,955.

Msimu huo 2005/06 Arsenal iliweza kufanya kazi kubwa nzuri. Iliweza kufika fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya. Michezo 12 bila ya kufungwa ikijumuisha rekodi mpya ya mashindano kutofungwa katika mechi 10 mfululizo, ikawawezesha Arsenal kumenyana na Barcelona katika fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya tarehe 17 mwezi wa Mei katika ndani ya Stade de France.

Licha ya Jens Lehman kupewa kadi nyekundu baada tu ya dakika 18 za mchezo, washika bunduki walikuwa wa kwanza kufunga bao kupitia Sol Campbell. Hata hivyo mwishoni mwa kipindi cha pili, Barcelona wakapachika mabao mawili na kuumiza mioyo ya mashabiki wa Arsenal waliofunga safari kuishangilia timu yao.

Ndani ya uwanja wa Emirates

Wakati klabu ikijiandaa kuhamia Emirates, nahodha wao na mfungaji bora kabisa katika historia ya klabu, Thierry Henry akaweka dhamira ya kubaki Arsenal kwa siku zijazo. Baadaye akiwa Ujerumani katika kombe la Dunia akaweza kuisaidia nchi yake kufika fainali. Mwezi wa saba 2006 klabu ikahama rasmi Highbury ambako ilidumu kwa miaka 93.

Dennis Bergkamp akacheza mechi yake ya mwisho kwa Arsenal na ya kwanza kabisa ndani ya uwanja mpya wa Emirates wakati Ajax Amsterdam inapambana na Arsenal katika mechi maalumu ya kumuaga mwanasoka huyo nguli.