Shakira kutumbuiza Kombe la Dunia

Mwanamuziki Shakira.
Image caption Shakira atanogesha Kombe la Dunia mwaka huu kwa wimbo maalum.

Wimbo ulioimbwa na Shakira kwa kushirikiana na kundi la muziki la Freshlyground kutoka Afrika ya Kusini umechaguliwa kuwa wimbo maalumu wa Kombe la Dunia mwaka huu.

Wimbo huo unaoitwa Time for Africa (Wakati wa Afrika) utaanza kusikilizwa kupitia vituo vya redio hivi karibuni na pia utakuwa ukipatikana kupitia mtandao wa intaneti.

Tarehe 10 mwezi Juni mjini Soweto, Shakira na Freshlyground watatumbuiza wimbo huo katika tamasha la uzinduzi kabla ya kuanza kwa michuano ya kombe la dunia.

Wimbo huo pia utaimbwa katika sherehe ya ufunguzi wa kombe hilo na siku ya fainali 11 mwezi wa saba.

Mwezi wa kwanza mwaka huu, Chama cha Soka cha England kilitangaza kuwa kwa mara ya kwanza mwaka huu toka 1966 hakutakuwa na wimbo maalumu wa kusindikiza kampeni ya England nchini Afrika Kusini.

Msemaji wa FA anasema hiyo ni kutokana na nia madhubuti ya menejimenti ya timu ya soka ya England kutaka kuweka nguvu na mawazo yote katika soka.

Zilizovuma

Nyimbo kadhaa zisizo rasmi tayari zinasikika sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ule ulioimbwa na John Barnes kwa fainali za kombe la dunia mwaka 1990, World in Motion by New Order.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England atashiriki katika kurekodi upya wimbo huo kwa ajili ya tangazo la televisheni.

Wimbo rasmi wa mwisho wa England katika Kombe la Dunia ulioitwa “World At Your Feet” wa kundi la Embrace ulikamata nafasi ya tatu katika chati za muziki mwaka 2006. Pia wanamuziki Tony Christie na Crazy Frog walifanya jitihada kadhaa za kutoa nyimbo za kuhamasisha kampeni ya England.

Mwaka 2002, wimbo “We are on the ball” ulirekodiwa na watangazaji wa TV, Ant na Dec.

Mwaka 1998, kundi la Spice Girls waliimba wimbo (How Does It feel To Be) On Top Of The World, ulioandikwa na Echo na Ian McCulloch wa kundi la Bunnymen