Beckham ajinoa kurejea uwanjani

David Beckham analenga kurejea dimbani mwezi wa Novemba atakapopona maumivu ya kisigino, hali iliyomfanya aondoke katika kikosi cha England cha Kombe la Dunia, Afrika Kusini.

Mwezi wa Machi ilitangazwa Beckham hatakanyaga dimbani kwa miezi sita lakini inaoneka kupona kwake kunachukua muda mrefu tofauti na ilivyotazamiwa.

Hali hiyo ina maana Beckham hatacheza michezo muhimu ya ligi ya Marekani msimu huu, labda tu Los Angeles Galaxy ifikie kucheza mechi za hatua ya mtoano.

Beckham amesema: "Sitaweza kukimbia kwa miezi mitatu ijayo, kwa hiyo huenda nikacheza tena soka mwezi wa Novemba."

Mchezo ambao anaweza kuichezea England ni wa kufuzu mashindano ya Ubingwa wa Mataifa ya Ulaya mwaka 2012, ambapo watacheza na Wales tarehe 29 mwezi wa Machi mwaka 2011.

Beckham alifanyiwa upasuaji mwezi wa Machi baada ya kuumia akichezea kwa mkopo AC Milan. Awali alisema angeweza kupona kabisa mwezi wa Septemba.

Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United bado anatembelea magongo hadi sasa.