Celtic wamtaka David James

David James
Image caption Kipa wa England

Kocha wa klabu ya Uskochi, Celtic, Neil Lennon, amesema anamfikiria David James kama mlinda lango atakayefaa kuchukua nafasi iliyowachwa wazi na Artur Boruc, na ana matumaini ya kumshawishi kujiunga na klabu.

Lennon tayari ana kipa Lukasz Zaluska kutoka Poland, na Mmarekani Dominic Cervi, lakini ana hamu sana ya kumsajili kipa maarufu, kufuatia Boruc kujiunga na Fiorentina.

"Itatuchukua muda, kwani bado tumo katika mashauri ya mapema tu", alielezea meneja huyo wa Celtic.

Klabu aliyokuwa akiichezea zamani James, Portsmouth, imeondoa ombi lake la kutaka kumsajili, na ambalo ililiwasilisha mwezi Mei.

James, mwenye umri wa miaka 39, aliichezea timu ya Pompey, (jina la utani la Portsmouth), katika mechi 138.

Kulingana na msimamizi wa Portsmouth, Andrew Andronikou, James alitaka kuwa mchezaji wa timu hiyo, na wakati huohuo kuwa ndiye meneja.

Steve Cotterill alipewa kibarua hicho cha meneja, na timu ya Portsmouth, ambayo huchezea uwanja wa Fratton Park, iliamua kuliondoa ombi hilo la kumtaka James, aliposhindwa kuonyesha angelipenda kuwa katika klabu hiyo.