Martin Jol akataa kibarua cha Fulham

Martin Jol ameamua kuikataa kazi ya umeneja katika klabu ya Fulham ya England, na ataendelea kuifundisha timu ya Ajax ya Uholanzi.

Image caption Kocha wa Ajax ya Uholanzi

Jol, mwenye umri wa miaka 54, awali alikuwa ameafikiana na Fulham kuhusu malipo na masuala mengine ya kibinafsi.

Fulham ilikuwa na mipango ya kumchukua kutokana na udhaifu wa kipengele fulani katika mkataba wake kinachohusiana na masharti juu ya kuihama Ajax.

Lakini klabu ya Fulham ilielezea kwamba mashauri kati yao na Ajax yamekwisha, kwani kipengele hicho hakipo tena.

Jol, kupitia wavuti ya Ajax amesema: "Ajax walinifahamisha kwamba hawataki niondoke. Sidhani ninaweza kuondoka wakati huu".

Aliongezea: "Nilifika hapa msimu wa joto uliopita nikitazamia ufanisi, kuimarisha timu, na pia kufurahi - hayo ndio mambo matatu ninatazamia kuyatimiza msimu ujao".

Klabu ya ligi kuu ya Premier ya Fulham imekuwa haina kocha tangu Roy Hodgson kujiunga na Liverpool, tarehe 1 mwezi Julai.

Fulham ilikuwa imemchagua Jol kuwa kocha wake mpya, na ilielekea kana kwamba mipango ilikuwa inaendelea vizuri, na Jol akionekana kutofurahia namna wachezaji walikuwa wakisajiliwa huko Uholanzi, na klabu ya Ajax ikiwa imepungukiwa kifedha.

Kulikuwa na uvumi kwamba pia huenda angelilazimika kumuuza mlinda lango Maarten Stekelenburg, mshambulizi Luis Suarez, na mlinzi Gregory van der Wiel msimu huu.

Lakini masuali mengi yalianza kujitokeza kuhusiana na mipango ya Fulham kumpata Jol, licha ya mkurugenzi mkuu Alistair Mackintosh kufunga safari ya Uholanzi kushauriana zaidi na Ajax.