Twiga Stars kupambana na Seattle

Wachezaji wa Twiga Stars na Northwest
Image caption Twiga Stars ilianza vyema kampeni yake Marekani

Timu ya taifa ya soka ya kina dada ya Tanzania, Twiga Stars, ambayo imekuwa ziarani nchini Marekani, Jumamosi, tarehe 7 Agosti, itacheza dhidi ya timu ya wanawake ya Seattle Sounders, ambao hucheza katika ligi ya 'USL W-League'.

Hii ni ligi daraja ya pili kwa kina dada.

Twiga Stars wanaitumia ziara hiyo kujiongezea maarifa kabla ya mashindano ya Afrika ya kina dada, yatakayofanyika nchini Afrika Kusini, mwezi Oktoba.

Awali, Jumatano, tarehe 4 Agosti, Twiga ilicheza mechi ya kirafiki na Northwest National Reds, ambayo ni timu ya vijana wa kike chini ya umri wa miaka 18, katika uwanja wa Starfire Sports Complex, kusini mwa Seattle, Washington.

Licha ya kusafiri kwa kipindi cha saa 28, na kuwasili usiku wa kuamikia mechi, Twiga Stars bado iliweza kuwashinda wapinzani wao magoli 2-0.

Magoli hayo yalifungwa na Eto Mlenzi na Esther "Lunyamila" Chabruma.

Northwest Nationals ni kati ya timu bora za soka katika jimbo la Washington, na wachezaji wake wengi kila msimu hupata nafasi ya kujishindia misaada ya kulipiwa mafunzo ya soka katika vyuo vikuu maarufu nchini Marekani.

Twiga Stars walifuzu kuingia mashindano hayo ya fainali, baada ya kuinyeshea Eritrea jumla ya magoli 11-3, na baadaye kuishinda Ethiopia magoli 4-2.